Bil. 1/- kuchangishwa matibabu moyo watoto

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 12:03 PM May 01 2024
Michango kusaidia watoto wenye magonjwa ya moyo.
PICHA: MAKTABA
Michango kusaidia watoto wenye magonjwa ya moyo.

TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Heart Team Africa Foundation (HTAF), imeandaa hafla ya kuchangisha Shilingi bilioni moja kwa ajili ya matibabu ya watoto.

Fedha hizo zinatarajiwa kukusanywa kutoka kwa wadau mbalimbali katika hafla itakayofanyika Julai 6, mwaka huu, wakati wa chakula cha hisani zitafanikisha  upasuaji wa moyo kwa watoto 500.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, ameyasema hayo jijini Dar es Salaam na kubainisha kuwa hatua hiyo inaunga mkono jitihada za serikali kuwatibu watoto wanaougua magonjwa ya moyo.

“Asilimia 70 ya gharama za matibabu kwa watoto huchangiwa na serikali. Pamoja na kuchangiwa, bado asilimia 80 hawamudu gharama hizo kwa asilimia 30 iliyobaki. Kiwango cha gharama kwa upasuaji kwa mtoto mmoja ni kati ya Sh. milioni nne hadi 15.

“Kwa mwaka, JKCI inafanya upasuaji kwa watoto 357.  Kwa  harambee hii tutaongeza upasuaji watoto kutoka idadi hiyo hadi watoto 500,” amesema Dk. Kisenge.

Amesema ushirikiano kati ya JKCI na HTAF ulianza mwaka jana kwa nia ya kusaidia watoto wenye magonjwa ya moyo na kuungana na serikali katika kusaidia matibabu ya watoto.

“Watoto wengi wanapata tatizo la moyo kwa kuzaliwa nalo na katika watoto 100 mmoja ana tatizo la moyo. Pia inakadiriwa nchini kwa wastani wa watoto milioni mbili wanaozaliwa kwa mwaka nchini, 13,000 hadi 14,000 kati yao wana tatizo hilo na 4,000 watahitaji upasuaji wa moyo,” ameongeza.

Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Moyo na Bingwa wa Magonjwa ya Moyo JKCI, Dk. Sulende Kubhoja,  amesema ongezeko la idadi ya watu nchini, linakwenda sambamba na idadi ya watoto wanaozaliwa na matatizo ya moyo.

“Mwaka 1962 Watanzania tulikuwa takribani milioni 10 na sasa ni milioni 61. Asilimia 60 nchini ni watoto walio na umri wa miaka 16. Asilimia 80 ya Watanzania ni walio katika umri wa miaka 40 ambao wako kwenye umri wa kuzaa.

“Kwa wastani watoto milioni mbili huzaliwa kila mwaka na katika hawa, kuna watoto takribani 10,000 wanazaliwa na tatizo la moyo na wengine watahitaji upasuaji. Upasuaji mmoja unaweza kufika Sh. milioni 15 hadi 20,”  amesema bingwa huyo.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa HTAF, Linda Gideon,  amesema lengo la kuandaa harambee hiyo ni kusaidia familia ambazo watoto wao wanaugua magonjwa ya moyo na kuhitaji upasuaji, huku hali zao zikiwa duni kifedha.

“Kwa mwaka huu taasisi inatarajia kukusanya fedha na kuwafanyia upasuaji watoto 200. Tunaomba wadau tofauti kutuunga mkono kwa kuchangia,”  amesema .