Kesi matunzo ya watoto zaongezeka

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 09:56 AM Apr 19 2024
Matunzo ya watoto.
PICHA: MAKTABA
Matunzo ya watoto.

KATI ya mashauri 14,600 yaliyoshughulikiwa ya migogoro ya ndoa yaliyohusu masuala ya kifamilia na matunzo ya watoto yanaongoza kwa asilimia 41.

Mashauri hayo yalipokewa kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 na yaliyohusu masuala hayo ni 5,944 sawa na asilimia 41, migogoro ya ndoa yalikuwa 5,306 sawa na asilimia 36 na matunzo ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa yalikuwa 3,350 sawa na asilimia 23.

Kutokana na hali hiyo, serikali imeelekeza mikoa na halmashauri kuandaa mijadala katika jamii kwa kutumia wataalamu wa malezi chanya ya watoto, familia, kuhusisha viongozi wa dini ili kutafuta ufumbuzi tatizo la malezi duni ya watoto na mmomonyoko wa maadili.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima akizungumza kuhusu maadhimisho ya siku ya kimataifa ya familia Mei 15, mwaka huu, amesema mashauri hayo yalifikishwa kupitia mabaraza ya kata na jumuiya na kwa mashauri 3,411 yalifikishwa kwa maofisa ustawi wa jamii 1,642 yalipatiwa ufumbuzi na 443 yanaendelea kufanyiwa kazi.

Amesema mashauri 1,326 yalipewa rufaa kwenda kwenye vyombo mbalimbali vya usuluhishi ikiwamo mahakama (921) na mabaraza ya kata na jumuiya (405).

Kadhalika, amesema taarifa ya utafiti wa hali ya afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria nchini ya mwaka 2022, inaonesha asilimia 27 ya wanawake wa umri wa miaka 15 hadi 49 walifanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili.

“Asilimia 12 ya wanawake wa umri huo walifanyiwa ukatili wa kingono, asilimia 13 ya wanawake waliowahi kuwa na mume au mtu mwenye mahusiano katika kipindi cha miezi 12 kabla ya utafiti huo walifanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili, kingono na kihisia,” amesema.

“Unyanyasaji wa kimwili, kingono, au kihisia miongoni mwa wanawake walioolewa umepungua kutoka asilimia 50 mwaka 2015/16 hadi asilimia 39, mwaka 2022/23.”

Ametaja moja ya vikwazo katika kukabiliana na migogoro ya familia ni kukosekana kwa upendo, ustahimilivu na kutokuwa na hofu ya Mungu miongoni mwa wanafamilia.

Aidha, amesema mifumo kandamizi inayoendelea katika jamii inayochochewa na mila na desturi za baadhi ya makabila nchini zimesababisha wanandoa hasa wanawake kukaa kimya bila kujadiliana na kumaliza tofauti zao jambo linaloweza kuwa na athari kubwa.

“Mara zote waathirika wakubwa huwa ni watoto. Vikwazo vingine ni uelewa mdogo kuhusu malezi chanya na mawasiliano duni miongoni mwa wanafamilia pamoja na wazazi kutotimiza majukumu yao ya misingi ya malezi. Changamoto hizi zimechochea mmomonyoko wa maadili,” amesema.

Amesisitiza wizara imeendelea kuratibu huduma za usuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia kupitia Baraza la Usuluhishi wa Ndoa la Kamishna wa Ustawi wa Jamii lililopo Makao Makuu ya Wizara.

Dk. Gwajima amesema, katika kuadhimisha siku hiyo aliwaomba viongozi wa dini watumie nyumba za ibada kutoa ujumbe kuhusu umuhimu wa malezi bora ya watoto kujenga familia imara na taifa imara.