Kinana amnadi Rais Samia kuleta maendeleo kwa usawa

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 08:06 PM Apr 18 2024

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana.
Picha: Maulid Mbagga
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana amemnadi Rais Samia Suluhu Hassan akisema anafanya mambo makubwa ya maendeleo kwa Watanzania ikiwamo kuongeza mapato ya serikali bila ya wananchi kushurutishwa au kuporwa fedha zao.

Akizungumza leo katika kikao kazi cha wanachama wa CCM Wilaya ya Musoma Mjini mkoani Mara, Kinana amesema chini ya uongozi wa Rais Samia nchi imepiga hatua kubwa ya maendeleo kuliko awamu nyingine zilizopita.

"Kwa nini tusitoe pongezi kwa Rais Samia?. Amefanya kazi nzuri, anajitoa, anajituma amekuwa kiongozi wa mfano anaongoza nchi yetu vizuri na maendeleo yanapatikana kila mahali na Musoma hapa ni mashahidi.

"Hata katika ukusanyaji wa mapato hakuna mwaka tumepata mapato makubwa bila kufunga watu, bila kupora watu kama mwaka huu. Huu ndio ukweli, Watanzania tumuunge mkono, kuna usemi unasema ukitaka jambo lisemwe mpe mwanaume ukitaka jambo lifanyike kwa uhodari mpe mwanamke.

"Kazi ya kusema ni ya mwanaume na kazi ya kutenda ni wanawake, akina mama ni waaminifu...Kwa hiyo Rais Samia  amefanya kazi nzuri lakini na Chama Cha Mapinduzi kinafanya mengi mazuri zaidi.

"Chama hiki ni kizuri, ukiona hakiendi ujue wakubwa huku juu wanakivuruga, sio wanachama," amesema Kinana na kufafanunua kuwa maendeleo yanayopatikana chini ya uongozi wa awamu ya sita yamefika hadi Musoma na Mkoa wa Mara kwa ujumla.

"Musoma hapo nyuma nikiwa Katibu Mkuu nilikuja kufanya ziara kulikuwa hakuna maendeleo kama ilivyo sasa. Mbunge  wa Musoma Mjini (Vedastus Matayo) ameeleza kuwa Musoma hamna shida ya barabara za lami, maana zipo.

"Shule ziko nyingi, maji yapo ya kutosha, hospitali ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere inaendelea vizuri, Rais amefanya mambo makubwa ya maendeleo," alisema Kinana.