Kinana: Serikali itachukua hatua kukabili athari mafuriko

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 09:27 PM Apr 19 2024
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana.
Picha: Maulid Mbagga
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana amesema Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa ujumla inafuatilia kwa karibu athari zinazotokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha sehemu mbalimbali nchini, huku zikisababisha uharibifu mali na miundombinu.

Amesema katika maeneo ambayo yanahitaji msaada wa dharura na haraka tayari serikali imeshachukua hatua ya kupeleka fedha za ukarabati wa miundombinu na misaada mbalimbali kuwasaidia walioathirika. 

Kinana ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wanachama wa CCM Wilaya ya Musoma Mjini ambao walieleza uharibifu wa baadhi ya miundombinu ya barabara katika wilaya hiyo na Mkoa wa Mara kwa ujumla  kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

"Serikali inaendelea kufanya tathmini ya uharibifu huo wa miundombinu ili kutenga fedha za kukarabati maeneo yote ambayo yameathirika. Uharibifu wa miundombinu umefanyika katika nchi mbalimbali duniani hata zile zilizopiga hatua kubwa ya maendeleo na sio Tanzania peke yake. 

"Kwa mara ya kwanza tumeona duniani nchi nyingi zimepatwa na mafuriko, hata zile ambazo katika historia hatukuwahi kuona mvua, hivyo sio sisi peke yetu, haya yote yametokana na mabadiliko ya tabianchi, mahitaji ya kufanya marekebisho ni makubwa na yataendelea," amesema Kinana.

"Niwaambie Rais Samia anapata taarifa kuhusu haya yanayotokea katika mikoa mingi, sehemu ambapo miundombinu imeharibika sana hadi kukosekana kwa mawasiliano hatua za dhati zimechukuliwa," amesema Kinana.