Maagizo 11 PM kuondoa vikwazo mazingira wezeshi wanahabari

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 07:16 AM May 04 2024
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ametoa maagizo 11, ikiwamo viongozi na wakuu wa taasisi zote kuondoa vikwazo vya utoaji taarifa kwa vyombo vya habari na kuweka mazingira wezeshi kwa wanahabari ili kuwarahisishia utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Majaliwa alitoa maagizo hayo jana jiji hapa, alipokuwa akizungumza kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.

Alisema wakuu wa taasisi wanapaswa kuondoa ukiritimba uliopo kwenye utoaji wa taarifa ili kuwezesha vyombo vya habari kutoa taarifa kwa wananchi. 

"Wakuu wa taasisi wote ondoeni ukiritimba wa utoaji wa habari kwa waandishi wa habari ili kuwezesha kupatikana kwa habari zenye viwango zinazohitajika na wananchi wetu lakini pia wekeni mazingira wezeshi na rafiki kwa wanahabari kupata habari," alisema Majaliwa  

Pia alisema usalama kwa waandishi wa habari wakati wa utekelezaji wa majuku yao ni jambo na muhimu, hivyo serikali itaendelea kusimamia kwa karibu jambo hilo. 

"Serikali itaendelea kusimamia suala la usalama wa waandishi wa habari ili kuhakikisha kuwa hakuna mwandishi wa habari hata mmoja anapata shida wakati wa utekelezaji wa majukumu yake," alisema 

Waziri Mkuu pia aliagiza maofisa wote wa serikali ambao wamekuwa na jukumu la kuratibu ziara za viongozi wa serikali, kuhakikisha waandishi wa habari wanakuwa na usafiri wa uhakika ili wasipate tabu kutekeleza majukumu yao.

 Pia alisema kutokana na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi duniani, vyombo vya habari vinapaswa kutumia nafasi yao kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira.

 "Tunalo jukumu la kuelimisha umma kuhusu utunzaji wa mazingira. Tunavyo  vyombo vingi lakini vingi haviandiki habari zinazohusu mazingira, hivyo kupitia majadiliano yenu, inabidi muone ni kwa namna gani habari za mazingira zinapewa uzito mkubwa ili kulinda mazingira," alisema.

 Alisema utafiti unaonyesha takribani watu milioni 16 nchini wanaoishi pembezoni mwa bahari, hivyo  maisha yao yanategemea rasilimali za baharini kwa hiyo kama mazingira yataharibiwa, maisha yao yatakuwa hatarini.

 "Lakini uharibifu wa mazingira unachangia kuongezeka kwa joto, magonjwa na takwimu zinasema kuwa asilimia 50 ya Watanzania bado wanatumia kuni na asilimia 20 wanatumia mkaa, hivyo lazima tuunge mkono juhudi za serikali kuhamasisha matumizi ya nishati safi," alisema.

 Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya, alisema katika maadhimisho ya mwaka huu, wamejadiliana mambo mbalimbali ikiwamo waandishi wa habari kuzingatia maadili.

 Simbaya pia alisema waandishi wahabari wanapaswa kutoa taarifa katika vyombo husika kila wanapokutana na vitendo vinavyo tishia usalama wao wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao ili hatua zichukuliwe.