Marekani kupambana malaria Tabora

By Halima Ikunji , Nipashe
Published at 11:18 AM May 01 2024
Marekani kupambana malaria mkoani Tabora.
PICHA: MAKTABA
Marekani kupambana malaria mkoani Tabora.

MFUKO wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Malaria (PMI) umeahidi kuongeza msaada wa utoaji huduma kwa Mkoa wa Tabora ili kupunguza kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo.

Hayo yamebainishwa na Mwakilishi wa Shirika la Misaada la Kimataifa Marekani (USAID) nchini, Lulu Msangi wakati akiwasilisha taarifa ya shirika hilo kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani yaliyofanyika Kitaifa mkoani hapa .

Lulu amesema kuwa mradi huo unaojulikana kwa jina la PMI Shinda Malaria utaanza kutekelezwa na Taasisi ya Ifakara Health Institute (IHI) kwa ufadhili ya USAID baada kuzinduliwa katika maadhimisho hayo.   

Amesisitiza kuwa msaada huo utajumuisha afua ya uchunguzi wa malaria na matibabu, afua ya mabadiliko ya tabia za kijamii, kuzuia malaria wakati wa ujauzito, ufuatiliaji na tathmini ya shughuli za kupambana na ugonjwa huo.

Lulu amebainisha kuwa shirika hilo halifurahishwi na kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo mkoani hapa kutokana na utafiti kubaini umewapata asilimia 23 ya watoto walio chini ya miaka mitano.

‘Hiki ni kiwango kikubwa sana cha malaria ukilinganisha na viwango vya mikoa  ya Singida, Manyara, na Dodoma ambayo ina asilimia moja tu ya watoto chini ya umri huo waliopatikana na ugonjwa huo,”  amesema.

Mkurugenzi wa Miradi Wizara ya Afya, Cathylene Joachim,  amesema serikali imeendelea kuweka mkazo na hamasa ya kudhibiti maambukizi hayo katika mkoa huo na mingine yenye kiwango kikubwa nchini.

Ametaja makundi mengine ambayo yako katika hatari kubwa ya kupata malaria kuwa ni wajawazito, wafanyakazi migodini, wavuvi na wakulima, hivyo wataendelea kuongeza hamasa zaidi kwenye matumizi ya vyandarua.

Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge Wanaharakati wa Kupambana na Malaria (TAPAMA), Riziki Lulinda, ameishauri serikali kuja na mkakati madhubuti wa kudhibiti ugonjwa huo mkoani hapa.

Akihitimisha maadhimisho hayo, Naibu Waziri wa Afya. Dk. Godwin Mollel amewataka wakazi wa Tabora na mikoa mingine nchini kutumia vyandarua na wanapohisi kuwa na malaria waende hospitalini.

Kwa mujibu wa Dk. Mollel, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameipatia wizara hiyo takriban Sh. tril. 6.7 kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo ili kuhakikisha kiwango kinashuka hadi asilimia 3.5.

Amesema kiwango cha malaria kinaendelea kupungua kila mwaka kwani mwaka 1990 maambukizi yalikuwa asilimia 50 lakini sasa wana asilimia 8.1 kitaifa licha ya mkoa huo kuwa na asilimia kubwa.