Matarajio mshahara, kikokotoo Mei Mosi

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 09:46 AM May 01 2024
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi (TUGHE), Hery Mkunda.
PICHA: MAKTABA
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi (TUGHE), Hery Mkunda.

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limesema matarajio ya wafanyakazi leo ni nyongeza ya mshahara ambao wanaamini ukiboreshwa vizuri mfanyakazi anapostaafu atapata mafao mazuri.

Kikubwa pia kinachosubiriwa ni kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kanuni mpya ya kikokotoo cha mafao ya wastaafu.

Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi, akijibu hoja mbalimbali za wabunge zilizoibuka bungeni, amesema suala la kanuni mpya ya kikokotoo cha mafao ya wastaafu litajulikana Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi).

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu kuhusu matarajio ya wafanyakazi leo, Makamu wa Rais wa TUCTA, Shabani Ambindwile,  amesema matarajio yao ni kusikia nyongeza ya mshahara ambayo wanaamini mfanyakazi akipata mzuri atapata mafao mazuri.

“Mfanyakazi akitengenezewa mshahara vizuri atapata mafao mazuri. Upandishaji madaraja ni jambo ambalo serikali hufanya kila mwaka. Suala la kikokotoo lina taratibu zake,”  amesema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi (TUGHE), Hery Mkunda,  amesema wana matarajio mengi kutoka serikalini na wao wanaahidi kuendelea kushirikiana nayo.

Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina baadhi ya wafanyakazi walisema, jambo kubwa wanalotaka kusikia ni nyongeza ya mshahara na suala la kikokotoo.

“Tunaamini Rais Samia atasikia kilio cha wafanyakazi. Tangu aingie madarakani tumeona mabadiliko kupitia uongozi wake, tunaamini atatufurahisha kesho (leo) Mei Mosi.

“Mambo mengine tunayotarajia kusikia ni suala la upandishaji wa madaraja na ajira mpya ambayo inalenga kundi kubwa la vijana waliomaliza ngazi mbalimbali za elimu ikiwamo vyuo vikuu mbalimbali,”  amesema.

Katika majibu yake bungeni, Katambi amesema serikali haiwezi kufumbia macho wala masikio suala la kikokotoo.

Akifafanua kauli yake kuwa, “Rais amaishatoa maelekezo zaidi ya mara mbili, kwamba tulifanyie mapitio upya kuona namna ya kukifanyia maboresho zaidi ili wastaafu wasipate shida, tayari tumeanza kazi hiyo na sheria inatutaka kufanyia maboresho kila baada ya miaka mitatu na tayari imepita.

…Tunaendelea kulifanyia kazi maana tumepokea maelekezo ya Rais pamoja na Bunge, lakini pengine tunaweza kusikia kauli ya Rais katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, siku ya Mei Mosi atakapokutana na wafanyakazi kueleza suala hili, hivyo tumelipa uzito unaostahili kuhakikisha tunaliweka sawa,” ameahidi.

Siku ya wafanyakazi hutumika kama sehemu ya kuwasilisha changamoto za wafanyakazi kwa mwajiri ili zipatiwe ufumbuzi.

Kilio kikubwa hasa kwa watu wanaostaafu kufanyakazi ni kikokotoo ambacho kinadaiwa hakiendani na muda waliotumia kufanyakazi.

Suala hilo pia limewaibua wabunge katika mijadala inayoendelea bungeni, mawaziri wanapowasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara zao.

Mbunge ambaye mara kwa mara husimama bungeni kulipambania ni Esther Bulaya (CHADEMA), ambaye anapinga kikokotoo cha asilimia 33 akitaka kirudishwe cha asilimia 50 ili wastaafu waweze kuishi maisha yasiyokuwa na mawazo.

Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, NSSF na PSSSF ndio yenye dhamana ya kuhifadhi michango ya wafanyakazi kwa kuifanyia miradi ya uzalishaji ya kuwanufaisha wanachama wake.