Samia awaomba wakuu IDA kutimiza ahadi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:43 AM Apr 30 2024
Rais Samia Suluhu Hassan akifurahia jambo na baadhi ya Watanzania waliofika kumpokea Jijini Nairobi.
PICHA: IKULU
Rais Samia Suluhu Hassan akifurahia jambo na baadhi ya Watanzania waliofika kumpokea Jijini Nairobi.

RAIS Samia Suluhu Hassan amewaomba wakuu wa Mfuko Maalum wa Benki ya Dunia unaotoa mikopo nafuu na misaada kwa nchi zinazoendelea (IDA), kutimiza ahadi zao ili kukuza maendeleo ya kiuchumi ya Afrika na kuboresha hali za maisha.

Pia, amesema Tanzania inaunga mkono IDA 21 wenye malengo yanayoendana na matarajio ya maendeleo ya Afrika na mahitaji ya rasilimali.

Ameyasema hayo nchini Kenya wakati akihutubia Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wenye lengo la kuainisha vipaumbele vya nchi hizo vizingatiwe katika mzunguko wa IDA 21.

Pamoja na mambo mengine, Rais Samia amewashukuru washirika wa IDA kwa msaada wao na kuwaomba waendelee kutimiza ahadi zao kwa nchi za Afrika.

Amesema nchi hizo zinahitaji kukua kwa na ujuzi wa kiteknolojia kama walivyojadili katika mkutano wa rasilimali watu uliondaliwa na nchi hiyo kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB) Julai, mwaka jana.

Amesema mkutano huo unafanyika katika kipindi ambacho Afrika na dunia zinakabiliwa na changamoto nyingi na upungufu wa ufadhili wa maendeleo na fedha na kwamba kuna haja ya mpango huo kuzingatia mahitaji hayo.

Amesema kwa kuzingatia changamoto ya viwango vya sasa vya madeni Afrika, IDA 21 inapaswa kuzingatia zaidi kutoa mikopo ya masharti nafuu, kama vile mikopo ya miaka 50.

“Kwa kuongezea, katika mzunguko ujao wa IDA 21, ni muhimu kwamba sera zirahisishwe na michakato ya uendeshaji iwe rahisi. Hili ni suala ambalo lina athari ya moja kwa moja juu ya upatikanaji wa fedha za maendeleo, gharama zisizo za moja kwa moja za fedha kufikiwa kwa malengo ya maendeleo ndani ya mfumo uliopangwa,” amesema Rais Samia.

Amesema katika mkutano wa IDA 20 ulioratibiwa na Tanzania ulijadili pamoja na mambo mengine athari za ufadhili wa mfuko huo na kusisitiza umuhimu wa maboresho katika IDA21.

Amesema Tanzania ni mnufaika wa mfuko huo ambao umesaidia kuboresha afya ya mama na mtoto, viwango vya umeme vijijini, upatikanaji wa maji safi ya kunywa na uhimilivu wa kiuchumi kwa upana zaidi.

“Kwa mfano, nchini Tanzania, tuna mradi wa miundombinu jijini Dar es Salaam unaoitwa Mradi wa Maendeleo ya Bonde la Msimbazi. Mradi huu ulinufaika na usaidizi wa Benki ya Dunia wa Dola za Marekani milioni mbili,” amesema Samia.

Amesema baada ya kupata rasilimali hizo, Tanzania tayari imepata Dola za Marekani milioni 60 kutoka kwa washirika wengine kwa ajili ya mradi huo, ambao unalenga kuimarisha uwezo wa kupambana na mafuriko na maendeleo jumuishi ya mijini katika kitovu cha kiuchumi.  

Naye Rais wa Kenya, Willium Ruto amesema mzigo wa madeni unaoongezeka kwa nchi za Afrika, athari za mabadiliko ya tabianchi na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona unaonyesha haja ya maboresho ya mpango huo.