Serikali kufuta NGOs zinazotenda kinyume na malengo ya usajili

By Zanura Mollel , Nipashe
Published at 10:12 PM Apr 18 2024
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Khamisi
Picha: Zanura Mollel
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Khamisi

SERIKALI imetishia kuyachukulia hatua kali ikiwemo kuyafungia na kuyafuta, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) ambayo yanaendesha shughuli zake kinyume na katiba zao, ambazo zimesajiliwa serikalini.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamisi, katika hafla ya uzinduzi wa utekelezaji wa Azimio la Itifaki ya Maputo, iliyoandaliwa na Jukwaa la Wanaelimu Wanawake wa Afrika, tawi la Tanzania (FAWETZ), jijini Dar es Salaam.

“Serikali inaagiza mashirika yote yaliyosajiliwa kufanyakazi kama zile walizoziandika katika utendaji wa kazi zao. Serikali haitasita kufungia mashirika yanayotekeleza majukumu ambayo hayapo kwenye usajili wenu," amesema Mwanaidi.

Hata hivyo amesema kuwa pamoja na kuwa mashirika yanajitahidi kumkomboa mtoto wa kike katika matukio ya kikatili lakini pia amehasa kutowasahau watoto wa kiume kwa kuwa nao wanapitia ukatili kutokana na mabadiliko ya dunia.

"Nchi imekumbwa na vitendo vya kikatili, watoto wa jinsi zote wanabakwa, tunapaswa kuondoa ukimya ili kutatua matatizo haya ya ukatili unaoibuka ndani ya jamii yetu,” amesema.