Wazazi wachangia wanafunzi kuwa watoro

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 10:16 AM May 01 2024
Wanafunzi wa shule ya msingi wakiwa shuleni.
PICHA MAKTABA
Wanafunzi wa shule ya msingi wakiwa shuleni.

BAADHI ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Ng’homango wilayani hapa wanadaiwa kukithiri kwa utoro kwa kuzuiwa na wazazi wao kwenda shule msimu wa kilimo.

Madai hayo yametolewa  na Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo, Peter Yuga wakati akizungumza na Nipashe shuleni hapo kuhusiana na mahudhurio ya wanafunzi.

Yuga, amesema katika msimu huo wa kilimo, baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwazuia kwenda watoto wao kwenda shule na kuwapeleka mashambani kulima.

Mtendaji wa Kijiji hicho cha Ng’homango, Madilya Nyema,  amesema kutokana na kukithiri kwa utoro wa wanafunzi msimu huu wa kilimo, waliitisha mkutano wa hadhara na kuwaonya wazazi kuwa mwanafunzi atakayekutwa shambani wakati wa masomo atatozwa faini ya Sh.10,000.

Nyema,  amesema licha ya kuweka faini hiyo wazazi waliendelea kukaidi amri hiyo na kuendelea kuwazuia watoto wao kwenda shule.

 Amesema kiasi cha fedha walizokuwa wakikusanya kwa kutoza faini hilo, zilielekezwa kwenye ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa shuleni hapo.

“Baada ya kuona wazazi wamekuwa vichwa ngumu na kuona faini hiyo ni kidogo, tukaamua kuongeza faini kuwa ni kupeleka shuleni hapo mifuko miwili ya saruji kwa kila kichwa cha mtoto, sasa hivi utoro umepungua siyo kama zamani,”  amesema.

 Baadhi ya wanafunzi shuleni hapo wamethibitisha baadhi ya wazazi kuwazuia kwenda shule msimu wa kilimo na kusababisha kukithiri kwa utoro.

Mmoja wa wazazi,  Razalo Masanyiwa,  amesema baadhi yao wanawazuia watoto kwenda shule ili wakalime mashambani wakati wa kilimo na mavuno kutokana na uchache wa watu kwenye familia.