Kibadeni katika ufalme wake Simba vs Yanga

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:51 AM Apr 22 2024
King Kibadeni Mputa akikinoa kikosi chake cha Simba.
Picha: Maktaba
King Kibadeni Mputa akikinoa kikosi chake cha Simba.

MIAKA 47 imepita tangu Abdallah 'King' Kibadeni, alipofunga mabao matatu 'hat-trick' kwenye mechi ya watani, 'Kariakoo Dabi', kati ya Simba na Yanga.

Hadi leo hii hakuna mchezaji yeyote si wa Simba au Yanga aliyefanya hivyo. Kibadeni akiwa amevaa jezi ya Simba namba 10, mgongoni akicheza nafasi hiyo, alifunga mabao matatu na kuiongoza timu yake kutoa kipigo kitakatifu cha mabao 6-0 kilichoingia kwenye historia ya 'dabi' na soka la Tanzania hadi leo hii.

Ilikuwa ni Julai 19, 1977 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam (sasa Uhuru), alipoweka rekodi hiyo, akifunga mabao dakika ya 10, 42 na 89, mengine mawili yakifungwa na Jumanne Hassan 'Masimenti' dakika ya 60 na 73, huku beki wa Yanga, Selemani Sanga akijifunga mwenyewe dakika ya 20.

Mechi hiyo imebaki kwenye rekodi ya kuwa, Kibadeni ndiye binadamu wa kwanza kufunga 'hat-trick' katika mechi ya watani ambayo hadi leo hii miaka 47 imepita haijavunjwa.

Wapo wachezaji waliokaribia kufanya hivyo wakifunga mabao mawili kwenye 'dabi; kama   Emmanuel Okwi, Hamis Kiiza, Jerry Tegete na hivi karibuni Max Nzengeli wa Yanga alitupia bao mbili, Novemba mwaka jana.

Kadiri miaka inavyozidi kusonga mbele haionekani dalili za kufikiwa au kuvunjwa kwa rekodi hiyo kutokana na idadi ndogo ya mabao ambayo yamekuwa yakifungwa na washambuliaji pindi timu hizo mbili kongwe zinapokutana.

Kitendawili kinabaki kuwa itachukua miaka mingapi hadi kuvunjwa kwa rekodi yake hiyo.

Mechi hiyo pia bado inasimama kuwa ndiyo mechi iliyotoa kipigo kikubwa zaidi katika mechi za 'dabi', mpaka sasa.

Nipashe limefika nyumbani kwa Kibadeni, Chanika jijini Dar es Salaam, na kuzungumza na mchezaji huyo wa zamani wa Simba na Timu ya taifa, Taifa Stars, ambaye jina lake halisi ni Abdallah Athumani Seif, lakini kutokana na umahiri wake kwenye soka mashabiki walimpachika majina mengine ambayo ni King Kibadeni Mputa', na kuongea naye juu ya mambo mbalimbali ya soka, tangu mchezaji hadi kuwa kocha.

King Kibadeni anaweka wazi mambo mbalimbali ikiwamo safari maisha yake ya sasa licha ya kutocheza, lakini anaishi katika soka akiwa na kituo chake cha KISA kilichopo katika mji wake huo.

 ATAKAYEMVUA UFALME WA HAT-TRICK

Kibadeni anasema bado anajivunia kwa miaka 47 sasa hakuna mtu ambaye amefanikiwa kufikia au kuvunja rekodi yake ya kufunga hat trick katika pambano la watani wa jadi.

“Watu wanatakiwa kukubali kuwa mimi bado ni mfalme, yeyote ambaye anataka kufikia au kuvunja rekodi yangu na kunipoka ufalme huu basi aje kwangu aniombe ni mpe baraka zangu.

"Atakayekuja kufuata baraka zangu basi tambua huyo ndiye atakayefikia na kuvunja rekodi hiyo iliyodumu takriban miaka 47 sasa tangu 1977,” anasema Kibadeni.

 

SABABU YA KUSHINDA BAO 6-0,  1977

“Unajua zamani tulikuwa tunaenda viwanjani kumuangalia mpinzani wetu tunayecheza naye hivi karibuni, nakumbuka kipindi hicho Simba tuliweka kambi Kibaha.

"Tukaenda Uwanja wa Karume, kuangalia Yanga inacheza na timu moja (hakumbuki jina), hiyo mechi walishinda bao 5-0,  siku hiyo wachezaji wa Yanga walituzomea na kutumwagi michanga.

"Kitendo hicho kilituumiza sana, tukarudi kambini na tulipomaliza kula chakula cha usiku mida ya saa mbili, wachezaji wote tulifanya kikao chetu na kupanga mipango yetu,” anasema.

Kibadeni anasema baada ya muda walikubaliana kila mchezaji mwenye gari alilipeleke uwanjani na kuwasha taa kwa ajili ya kupata mwanga na kuweza kufanya mazoezi usiku huo.

“Tulifanikiwa sana nakumbuka ilikuwa bado siku mbili kucheza na Yanga, tuliendelea kufanya mazoezi usiku huo, siku ya pili ilikuwa kazi ni hiyo dhamira yetu ni kuhakikisha tunalipa kisasi cha kumwagiwa michanga na kule kutuzomea,” anaeleza mfalme huyo wa hat-trick katika mchezo wa Derby.

Anasema wachezaji wenzake walimuahidi kutengeneza nafasi na kazi yake kubwa kufunga, anakumbuka bao la sita katika mchezo huo pasi ya bao aliipokea kutoka kwa Abbas Dilunga.

 

FIGISU ZA MECHI NA YANGA 2013

“Hii ni mechi ambayo sitaisahau kwa sababu kulikuwa na mambo mengi nje ya uwanja, nakumbuka wakati tunajiandaa na mchezo huu tulienda kuweka kambi Kigamboni (Bamba Beach).

Kuna baadhi ya viongozi walikuja kwangu na kuniambia nisiruhusu kiongozi yeyote kuingia kambini kwa sababu walikuwa wakirubuni wachezaji,” anasema.

Kibadeni anasema kwa kuwa viongozi hao waliniambia maneno hayo ndio hao hao walikuwa wakija kuzungumza na wachezaji akawa anapata wakati mgumu kwa sababu walifanya hivyo ili kuonekana uongozi haufai na wajiuzulu.

“Kabla ya mechi nilipewa majina ya wachezaji hao na niliwapanga kikosi cha kwanza lengo langu likiwa ni kuthibitisha niliyoambiwa. Ni kweli maana hadi tunaenda mapumziko tayari tuko nyuma kwa mabao 3-0 nilikuwa katika hali mbaya sana.

Ila nilipoingia katika chumba cha kubadilisha nguo niliwaeleza wasaliti na kuwapa nafasi vijana wadogo kutoka kwenye timu yetu ya vinaja, akiwamo Galaxy (William Lucian), Jonas Mkude, Said Ndemla, Ramadhani Singano na wengine ,” anaeleza Kibadeni.

Anasema aliwapa maelekezo madogo na kuwaamini wakafanye kile alichowapa kwenye uwanja wa mazoezi na kufanikiwa katika dakika 45 ya kipindi cha pili tukafanikiwa kusawazisha na waliwakosa kuwafunga bao la nne.

 

KISA SIMBA AKOSA RAHA KWENYE MJI WAKE

“Hapa Chanika watu wote wananifahamu kuwa ni Simba, hivyo inapofanya vibaya nakosa amani na raha kwa sababu ya Simba wenzangu huja kuniuliza maswali mengi na wengine Yanga kunizodoa.

Hali hiyo ikanifanya niichukie kuangalia mpira na kuisusa Luninga na kutoangalia kabisa Simba kwa sababu ya kuepukana na maumivu hasa pale napoangalia na kufungwa,” anasema kocha huyo.

 

KUTOSHIRIKISHWA KWA NYOTA WA ZAMANI

Anaeleza kwamba licha ya wachezaji wa zamani kucheza kwa mafanikio, lakini wamewekwa nyuma na viongozi kwa kutopewa nafasi ya kutoa michango yao ikiwamo kupata nafasi ya kuzungumza na wachezaji, lakini kutoa mawazo  juu ya timu yao.

“Unajua miaka ya sasa ni tofauti,  zamani wachezaji tulikuwa tunajuana ukiharibu uwanjani unamfuata nyumbani kwake kumueleza. Sasa hivi tumekuwa na mchanganyiko wa wachezaji wazawa na wakigeni.

"Wakigeni wanakuja kwa ajili ya kazi mapenzi ya timu si sana, tofauti na wazawa hawa wanacheza kama kazi, lakini na mahaba, katika hilo kama wachezaji wa zamani inapofika mechi kubwa tunatakiwa kuzungumza nao kwa sababu kuna mambo mengi yanapita,” anasema.

Kibadeni anasema kuna watu ambao wapo ndani ya Simba, lakini wanaumia timu inapofanya vizuri ba kufurahi inapoharibikiwa kipindi hicho ndicho cha kuweza kuzungumza na wachezaji kutorubuniwa.

 

MFALME NDANI YA SIMBA SASA

Licha ya kiungo Clatous Chama kuimbwa kuwa ni mfalme wa Wekundu wa Msimbazi hao, lakini Kibadeni yuko tofauti na maono ya Wanasimba kwa kudai kwa sasa bado hajamuona mfalme ndani ya klabu hiyo.

“Chama ni mchezaji mzuri sana, lakini bado hajafikia ule ufalme niliokuwa nao kipindi changu, kwa sababu wachezaji wa sasa wanacheza mechi kwa vipindi, atakuonyesha mchezo mzuri mechi moja inayofuata hataonyesha kiwango kile,” anasema nyota huyo wa zamani.

 

SABABU YA KUPOTEA KWA SIMBA

Kibadeni anasema kuna mambo mengi hufanya timu hiyo kushindwa kuonyesha ubora wao wa misimu minne iliyopita ikiwamo kutokuwa wamoja.

“Ile kaulimbiu yetu ya 'Simba Nguvu Moja' haipo kwa sababu hatuko wamoja, baadhi ya watu  waliopo ndani ya Simba, wanafurahi kuona timu inafanya vibaya, kwa mtindo huo ninaimani itakuwa ngumu kwetu kupata ubingwa kwa msimu huu,” anahitimisha Kibadeni.