Mjane mwenye umri mdogo zaidi nchini arejeshwa shule

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 10:19 AM Mar 26 2024
Mwanafunzi.
PICHA: BBC
Mwanafunzi.

SHERIA ya Ulinzi wa Mtoto ya Mwaka 2009 inamtambua mtoto hadi umri wa miaka 18, lakini licha ya kuwapo kwa sheria hii, mtoto mwenye umri wa miaka 11 ameozwa, baada ya miaka mitano, akiwa mjane.

Idadi ya wajane Tanzania imefikia  1,396,262, kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022." amesema Waziri Dorothy Gwajima

Ni binti wa jamii ya Kimang’ati (jina tunahifadhi) ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 17. Alifiwa na mumewe mwaka 2022, mwaka uliofuata akajiunga Chama cha Wanawake Wajane Tanzania (CCWWT) akiwa tayari na watoto wawili wa mwisho mwenye miaka mitatu.

Katika mazungumzo na mwandishi wa habari hizi, Katibu wa chama hicho, Sabrina Tenganamba, anasimulia kisa hicho, akisema kuwa mwanachama wao huyo ndiye mwenye umri mdogo. Mwanachama mwenye mkubwa kuliko wote ni mwenye miaka 90.

Akisimulia safari yake, Sabrina anasema kuwa mwaka 2023 walimpokea binti huyo kuwa mwanachama wao baada ya kuwatafuta kutokana na changamoto zilizokuwa zinamkabili.

“Anatoka jamii ya wafugaji sehemu moja inaitwa Forest,  Mkoa wa Pwani, ana watoto wawili. Kesi yake ilikuwa baada ya kufiwa na mume wake kulingana na tamaduni zao, akarithiwa.

“Maisha yake baada ya kurithiwa yakabadilika, akawa si mama wa kulea watoto tena, muda mwingi ulikuwa ni kushinda na mifugo porini. Katika maelezo yake alituambia nilijiona kama mtumwa kule porini. Nimewatafuta kuwaomba mnisaidie'. 

"Kama nilivyokueleza mwandishi, chama chetu kipo mikoa mbalimbali, huwa tunatembelea maeneo tofauti. Alitueleza hana nyumba wala pa kukaa kwa sababu kule kwao ni porini, wanamiliki ng’ombe tu. Na kwa mujibu wa tamaduni zao, yeye kama mwanamke wa wafugaji si mmiliki wa hiyo mifugo, hana fursa binafsi ya kumiliki ng’ombe.

“Alitusimulia changamoto zake nyingi ikiwa ni pamoja na kukosa fursa ya kwenda shuleni. Tukamwuliza kwa wakati huo anataka nini? Tulijua angetuambia ujasiriamali kutokana na jukumu la malezi alilonalo, lakini yeye akawa tofauti, akasema anataka kusoma," anasimulia katibu huyo.

Sabrina anasema wanachama wao wengi wanapowapokea huangukia katika ujasiriamali, lakini kwa mjane huyo ilikuwa tofauti. 

“Yeye akawa tofauti, akatuambia anataka kusoma, yaani kuanza elimu ya msingi. Kwa kuwa, mimi nina ofisi Bagamoyo na ni mchungaji, hivyo chama kikaamua kumpeleka shule na watoto wake nikawachukua ili mama yao apate muda wa kutosha wa kujisomea kutimiza ndoto yake ya kupata elimu,” anasema.

Sabrina anabainisha kuwa binti huyo kwa sasa anaishi makao ya nyumba salama huko Pwani na anasoma kupitia Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Wanaokosa (MEMKWA) na kutokana na maendeleo mazuri darasani, amevushwa hadi darasa la sita.

Sabrina anafafanua kuwa chama chao, pamoja na mambo mengine, hulenga kusaidia wanawake wajane kutimiza ndoto zao kulingana na hali zao, lengo ni kujikwamua kiuchumi na kutunza familia walizoachiwa.

KILIO CHAO

Sabrina anaomba serikali kupitia taasisi zake za fedha pamoja na sekta binafsi zinazotoa mikopo yenye riba nafuu, wasaidie wajane wanaofanya biashara ndogo kwa kupunguza riba za mikopo ili wanufaike na kukuza biashara.

“Hizi riba za kausha damu tutapoteza wajane wengi na tutapoteza taifa kwa ujumla ambalo ni kundi la watoto wanaoachwa baada ya baba zao kufariki dunia. Wanajikuta katika malezi ya upande mmoja, tena kwa mwanamke asiye na kipato na mwingine akiwa hana mali,” anasema.

Katibu huyo anasema chama chao kina mwanasaikolojia ambaye huwasaidia wajane ambao huingia ndani ya chama wakiwa hawana mwelekeo wa maisha huku wakiwa wamekata tamaa kutokana na madhila waliyokutana nayo baada ya kufiwa na kuhitaji ushauri kutoka kwa msaikolojia.

“Msaikolojia hukaa nao mpaka wakae vizuri na wanapoonesha kupona yale yanayowanasibu ndipo chama kinachukua jukumu lake la kuwasaidia kufikia malengo yao.

“Wengine tunawaunganisha na wafanyabiashara wadogo, mfano wanaotengeneza batiki, wanajifunza na baadaye wanakuwa wajasiriamali,” anasema.

MSAIKOLOJIA ALONGA

Lucas Sanga, msaikolojia tiba, anayetoa msaada wa kisaikolojia kwa wajane katika chama hicho anataja changamoto kubwa anazokutana nazo mara kwa mara na namna anavyozitatua.

Sanga anasema wengi anaokutana nao huwa wamekata tamaa kwa kuwa walikuwa wanategemea waume zao kwa asilimia kubwa na hawakuweka utaratibu wa kusimama wenyewe.

“Wapo ambao hufikiri ujane ni ulemavu na wanatamani kuonewa huruma. Wengi wanaofika kwangu wanakuwa wameingia katika migogoro ya kifamilia na ndugu upande wa mume, baadhi wanakuwa wamekata tamaa kwa kuhofia kurogwa na kuogopa kupigania haki zao,” anasema.

Sanga anasema kwa wajane wenye umri mkubwa baadhi hufika kwake wakiwa katika hali ngumu kiafya kutokana na kushambuliwa na magonjwa kama presha, sukari, saratani na baadhi huwa na hofu ya kwenda hospitalini kupima baada ya waume zao kufariki dunia kutokana na Upungufu wa Kinga Mwilini (UKIMWI).

“Wanakuja kwangu wakiwa na hofu ya kwenda kupima ili kujua hali za afya zao. Wanapokuja huwa ninawasaidia kwa kuwapa ushauri na mwishowe kuchukua hatua ya kwenda hospitalini,” anasema.

Msaikolojia Sanga anasimulia moja ya visa alivyokutana navyo ni mjane ambaye watoto wake pamoja na ndugu wa mume wake waliungana na kumtuhumu kuhusika na kifo cha mumewe na hivyo kufikia hatua ya kumnyang’anya baadhi ya mali.

“Bahati nzuri hawakuchukua nyumba. Alikuwa amekata tamaa, lakini nilimsaidia na sasa anajishughulisha na ufugaji wa kuku. Tulimpatia kuku 50 kama mtaji wake na kwa sasa anaendelea vizuri,” anasema.

HATUA SERIKALINI

Novemba 12, 2022, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, wakati akizindua Chama cha Wanawake Wajane Tanzania Tawi la Mkoa wa Dar es Salaam, alisema kwa mwaka 2020, Ofisi ya Takwimu Tanzania ilikadiria kuwapo wajane 880,000 ambao ni sawa na asilimia 3.1 ya wanawake wote ambao mwaka huo walikadiriwa kuwa ni milioni 28.5.

Katika maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani mwaka 2023, Waziri Gwajima alisema idadi ya wajane Tanzania imefikia  1,396,262, kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.

Alisema takwimu za duniani zinaonesha kuwapo wajane takribani milioni 258 na kati yao, wajane milioni 115 wanadhulumiwa, wanafanyiwa ukatili, wanakabiliwa na umaskini na kutengwa na jamii.

Waziri Gwajima alisema kuwa mbali na kutambua Siku ya Wajane Duniani, Serikali ya Tanzania pia imeweka mifumo ya kulinda haki zao na kuongeza huduma za msaada wa kisheria kwa kutungwa Sheria ya Msaada wa Kisheria Na. 1 ya Mwaka 2017.

Alisema kuwa mwaka 2021, serikali ilitoa msaada wa kisheria kwa wajane ambapo kesi 277 za miradhi zilitolewa hukumu  ya ushindi ikiwa ni pamoja na uendeshaji mashauri na hukumu katika utetezi wa haki.

Pia alisema kumeanzishwa madawati ya jinsia na watoto 420 katika vituo vya Jeshi la Polisi na vituo 153 katika Jeshi la Magereza kwa lengo la kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa waathirika, wakiwamo wajane.

Kampeni ya Maadili Yetu Taifa Letu - Kuwatunza na Kuwalinda Wajane ni Moja ya Maadili Yetu’ aliitaja ni sehemu ya mikakati ya kutoa elimu kwa jamii kuachana na ukatili wa kijinsia kwa kushirikisha wanaume.

Vilevile, Waziri Gwajima alisema wizara inaendelea kuratibu Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) ambao katika kipindi cha Julai 2022 hadi Aprili 2023, mikopo yenye thamani ya Sh. milioni 664.5 ilitolewa kwa wanawake wajasiamali 104, wakiwamo wajane.

Pia alisema Sheria ya Ardhi ya Kijiji Na. 5 ya Mwaka 1999, Kifungu cha 20(1), inatoa nafasi kwa wanawake, wakiwamo wajane kumiliki ardhi.

Alisema serikali pia inatekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA 2017/18-2021/22), wakiwamo wajane.

Siku ya Wajane Duniani huadhimishwa Juni 23 kila mwaka. Siku hii iliasisiwa na Lord Loomba, mwanzilishi wa Loomba Foundation mwaka 2005 baada ya baba yake kufariki dunia Juni 23, 1954.

Umoja wa Mataifa ulipitisha siku hiyo kuwa ya kimataifa kupitia Azimio Na. A/RES/65/189 la Desemba 21, 2010 ambayo hutoa fursa kwa wajane na wadau kutafakari mipango, mikakati, mafanikio na changamoto wanazokumbana nazo kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika kuzitatua.