Vyama vyakosoa kebehi za Tundu Lissu

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 09:37 AM May 08 2024
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHAHEMA), Tundu lissu.
Picha: Maktaba
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHAHEMA), Tundu lissu.

BAADHI ya vyama vya siasa vimelaani kauli iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHAHEMA), Tundu lissu, kwenye majukwaa.

Vimesema kauli za kiongozi huyo ni za kebehi, chuki na kuidhihaki serikali na viongozi wake.

Akizungumza na waandishi wa habari visiwani Zanzibar, Mwakilikishi wa mwavuli wa vyama 11 vya siasa, Juma Ali Khatib amesema kiongozi huyo hana nia njema kwa Watanzania kutokana na kuhubiri kauli za kibaguzi hasa kwa upande wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Amesema Watanzania wana maadili yao, wakiongozwa na mila, silka na utamaduni katika misingi ya kuheshimiana na ndiyo sifa ya Mtanzania.

Juma ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha ADA Tadea, amesema asili ya Tanzania linatokana na muunganiko wa wananchi wa pande mbili zilizokuwa huru pamoja na undugu wa damu wa mataifa mawili, hivyo siyo vyema kiongozi huyo kukebehi upande mmoja wa muungano huo.

Aidha, amesema Watanzania wamejengwa na misingi ya uhuru katika nchi yao pasipo na mipaka, Mzanzibar kufanya kazi Tanzania Bara au Mtanzania Bara kufanya kazi Zanzibar hakuna kosa kisheria.

Hivyo, amemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini achukuwe hatua kwa mujibu wa sheria za vyama na vyombo vya ulinzi na usalama dhidi ya mwanasiasa huyo ili kuwa fundisho kwa watu wengine.

Amesema lengo la Rais Samia Suluhu Hassan kufungua mikutano ya kisiasa ili viongozi wa vyama vya siasa kuendelea kunadi sera zao siyo kuzungumzia kauli za uchochezi ni kufanya mikutano ya kistaarabu.

Naye Haji Ambari kutoka Chama cha NCCR, amesema wakati huu Tanzania ikifikisha miaka 60 ya muungano siyo vyema kuzungumzia chuki za kuwagawa Watanzania bila ya sababu ya msingi au kwa uroho wa madaraka ya mtu fulani.

Amesema wakati umefika kwa Watanzania kutokukubali kugawanywa na wanasiasa ambao hawana nia njema kwa taifa lao hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuendelea kuhubiri umoja na ushikamano uliopo.