MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA ) Kanda ya Magharibi, inatarajia kuanza msako wa wafanyabiashara wa mafuta kwenye vidumu na mapipa hivi kwa kukiuka sheria na kuhatarisha maisha ya wananchi.
Msako huo umetangazwa na Meneja wa EWURA wa Kanda hiyo, Walter Chirstopher, wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa ili kudhibiti biashara hiyo na madhara yake katika jamii.
Christopher amesisitiza kuwa wafanyabiashara hao wa mafuta aina ya petrol, diseli na taa wanatakiwa kutambua kuwa siku zao zinahesabika na kuonya kuwa wakikamatwa watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kukiuka sheria za mamlaka hiyo na kuhatarisha maisha ya wananchi kwenye maeneo yao.
“Sheria ya mafuta ya mwaka 2015 kifungu cha 131 inasema mtu yoyote haruhusiwi kuuza mafuta hayo bila kuwa na leseni kutoka EWURA,” amesema na kufafanua kuwa: “ Masharti ya EWURA mfanyabiashara anayotakiwa kutimiza ni kuwa na leseni na kujenga kituo cha mafuta."
Mhandisi Mwandamizi wa Mafuta wa EWURA, Ibrahimu Kajugusi, amesema mamlaka hiyo imepunguza masharti ya kuanzisha biashara hiyo na kwamba taratibu ziko wazi kwa mfanyabiashara anayetaka gharama za uanzishwaji vituo kwa vijijini zimeainishwa.
“Kwa taarifa ya Aprili 30, mwaka huu tulikuwa na vituo vya mafuta 464 vilivyojenga vijijini nchini nzima kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi na kuondokana na biashara ya kuuza mafuta kwenye chupa za maji ndani ya makazi ya watu, tunaendelea kuweka mazingira wezeshi ili viendelee kujengwa zaidi,” amesema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED