Madai fedha chafu za CHADEMA kuchunguzwa

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 01:36 PM May 08 2024
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni.
Picha: Maktaba
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), imesema bado inaendelea kuchunguza madai ya fedha chafu ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), yaliyotolewa na Makamu Mwenyekiti Bara, Tundu Lissu, Mei 3, mwaka huu.

Nipashe imemtafuta Mkuu wa TAKUKURU nchini, Salum Hamdani kutaka kujua uchunguzi wa jambo hilo umefikia wapi baada ya TAKUKURU kutangaza kufanya uchunguzi baada ya kiongozi huyo kutoa shutuma dhidi ya chama chake akiwa kwenye mkutano wa hadhara mjini Iringa.

“Uchunguzi ni ‘process’ na inachukua muda, kwa hiyo taarifa tumeipokea na tunaifanyia kazi, siwezi kusema itachukua muda gani lakini tunaifanyia kazi,” amesema Hamduni.

Aidha, katika ukurasa wa X, Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema aliyenukuu kauli iliyoandikwa na mmoja wa wanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania, Bob Wangwe.

Katika akaunti yake ya X, Lema aliandika kwamba, “Nimeona andiko la BOB Wangwe na maandiko mengine ya watu wengi pamoja na ushauri wake.”

“Jibu langu kwenu ni hili, tukiwa Arusha mahali fulani kwenye mazungumzo yetu ambapo nilikuwapo pamoja na kamanda Heche, Msigwa na Mwenyekiti Mbowe, Lissu aliongea maneno haya nanukuu “Kaka, Mwenyekiti, ulibeba chupa ya damu nisife wakati nimeshambuliwa kutoka Dodoma ukiwa umesimama kwenye ndege mpaka Nairobi.”

“Na ulikaa Nairobi na wenzako hawa muda wote wa matibabu yangu, siwezi kuchukua fomu utakayogusa kwenye chama hiki, tusiruhusu wapambe watuharibie chama.”

Lema ameandika kwamba maneno hayo aliwahi kuyasema Lissu wakiwa na John Heche, Peter Msigwa na Ezekiel Wenje pamoja na Mbowe.

Aidha, amesema hakuna vita kwenye nafasi ya urais ndani ya CHADEMA isipokuwa kuna wapambe hasa katika mwelekeo wa siasa wa mwaka 2024 na 2025.

Katika ukurasa wake wa X, Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Kichama Kinondoni ameandika: “Kelele za WanaCCM dhidi ya CHADEMA ni jambo la kawaida kwenye siasa za ushindani. CCM haiwezi kushambulia chama kingine cha siasa zaidi ya CHADEMA kwa kuwa inajua CHADEMA ndiyo tishio kwao. Hivyo hivyo kwa CHADEMA haiwezi kuhangaika na vyama vingine isipokuwa CCM. Tuishi humu.”

Hoja ya Lema na Kileo imekuja kukiwa na mjadala mitandaoni kuhusu kauli zilizotolewa na Lissu hivi karibuni na mojawapo akidai kwamba ndani ya chama hicho kuna fedha chafu.

Akiwa katika moja ya mikutano yake hivi karibuni mkoani Iringa, Lissu ametamka kauli hiyo akidai kwamba fedha hizo chafu hazijulikani zimetoka wapi.

“Kuna mtafaruku mkubwa sana wa uchaguzi ndani ya chama chetu. Kuna pesa nyingi ajabu kwenye uchaguzi huu, hela ambayo tukisema tufanye mikutano, tutafute vyombo vya matangazo huwa haipo. 

“Leo kwenye uchaguzi kuna hela ya ajabu, nyinyi mnafikiri hii hela ni ya wapi, mnafikiri hii hela itatuacha salama? Ukitaka kujua hatuko salama fuatilia mitandaoni, hizo pesa si za CHADEMA kwa sababu sisi huwa hatuna hela zozote,” amesema Lissu.

Kwa sasa chama hicho kinaendelea na chaguzi za ndani ya chama katika ngazi ya kanda ambazo baadhi zimeonyesha kuwa na ushindani mkali na wanaojadili mtandaoni wanasema huenda wagombea kwenye kanda husika wana majibu ya kauli hiyo ya Lissu.

Baadhi ya Kanda za CHADEMA zinazotarajia kuwa na uchaguzi ni Kanda ya Nyasa, Victoria, Kati, Kusini, Kaskazini, Pwani na Magharibi.

Kati ya hizo, Kanda ya Nyasa ndio inaonekana kuwa na ushindani mkubwa zaidi kutokana na kushindanisha vigogo wenye mvuto kwenye siasa ambao ni Joseph Mbilinyi maarufu ‘Sugu’, Peter Msigwa ambaye anatetea nafasi yake kwa mara nyingine kwenye kanda hiyo.

Sugu na Msigwa wote walishawahi kuwa wabunge kabla ya kura zao kupungua katika uchaguzi mkuu wa 2020.

Baada ya kukamilika uchaguzi wa kanda utafuatiwa na uchaguzi wa taifa ambao unamvutano kwenye nafasi ya uenyekiti taifa, ambaye kwa sasa ni Freeman Mbowe ambaye bado hajaweka hadharani kama ataendelea na nafasi hiyo au la.

Duru za siasa ndani ya chama hicho, zinaeleza kuwa Mbowe anampango wa kuendelea na uenyekiti hivyo atachukua fomu kugombea nafasi hiyo, huku wengine wakidai Lissu naye anaitaka nafasi hiyo jambo linalosababisha joto la uchaguzi huo wa ndani kuongezeka.