Mwanafunzi akutwa amejinyonga uwanjani

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 09:53 AM May 08 2024
Mwanafunzi akutwa amejinyonga uwanjani.
Picha: Maktaba
Mwanafunzi akutwa amejinyonga uwanjani.

MWANAFUNZI wa darasa la tatu wa Shule ya Msingi Lungwa iliyoko Kijiji cha Utengule Kata ya Utengule Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani hapa, Prince Mtivike (9), amefariki dunia baada ya kudaiwa kujinyonga kwa kamba ya viatu pembezoni mwa uwanja wa mpira shuleni hapo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga, amesema kuwa Prince  alikutwa akiwa amejinyonga muda mfupi baada ya kula chakula cha mchana na wanafunzi wenzake shuleni hapo.

Mkuu wa Shule hiyo, Erick Nyongole amelithibitishia Nipashe kuwa, mwanafunzi huyo amekutwa akiwa amekufa kwa kujinyonga pembezoni mwa uwanja huo.

Nyongole, amesema alipata taarifa kutoka kwa wanafunzi waliokuwa wakicheza na Prince  kuwa mwenzao huyo amekufa kujinyonga pembezoni mwa uwanja huo.

Baba mkubwa wa mtoto huyo, Alex Mtivike, amesema taarifa za kifo cha mtoto wao walizipata wakiwa mjini Makambako kutoka kwa baba yake mzazi.

Amesema  mtoto wao huyo alikuwa na tabia ya kutoroka nyumbani na kukaa mtaani hata kwa siku tatu na kurudi kwao.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Utengule, Antony Myava na Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo, Evaristo Mwinami wamewataka wazazi kuwa karibu na watoto wao ili kujua changamoto zinazowakabili.

Baadhi ya wakazi wa Utengule, walielezea kusikitishwa na tukio la mwanafunzi huyo kujinyonga na kuahidi kuendelea kuwa karibu na watoto ili kujua changamoto zao ili kudhibiti matukio mabaya likiwamo la kujiua.