Mbwambo mkono wa ‘kielektroniki’ unaowagusa watoto waliosahaulika

By Getrude Mpezya , Nipashe
Published at 11:48 AM Apr 23 2024
Fredrick Mbwambo, (kulia) katika moja ya mikusanyiko ya kijamii.
Picha: Getrude Mpezya
Fredrick Mbwambo, (kulia) katika moja ya mikusanyiko ya kijamii.

FREDRICK Mbwambo, ni kijana aliyezaliwa kwenye familia ya kawaida, lakini anayesukumwa na kujali wengine, kuwainua akitumia kidogo alichonacho kuwapa kesho iliyo bora.

Anaamini kumcha Mungu, kumpenda jirani na jitihada binafsi kuwa ndizo silaha za kumfanikisha kufikia popote kuanzia mahala alipo leo na atakapokuwa baadaye.

Mbwambo alipata elimu ya ualimu katika Chuo cha Kinampanda mkoani Singida na kuajiriwa kufundisha katika Shule ya Msingi Nyamadoke iliyoko Sengerema anakoanzia kazi ya kushika chaki darasani.

Anafanyakazi kwa muda na kujiendeleza zaidi, akisoma  hadi  kidato cha  sita  na kujiunga na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na kwa sasa ni mwanafunzi wa kozi ya uhusiano wa kimataifa na diplomasia jijini  Arusha.

 Anaamini kuwa ni lazima kujituma, kujitolea na kutumikia jamii. Leo Mbwambo amejitwisha majukumu muhimu, baada ya kuanzisha Taasisi ya Gentech Foundation inayojihusisha na ustawi na kutoa elimu ya teknolojia, vifaa kama vile kompyuta za mezani na mpakato na vishikwambi (tablets) kuwawawezesha watoto wasio na uwezo kujifunza sambamba na kuwapatia vifaa vya  michezo kama mipira na jezi ili washiriki michezo.

 Amewafikia watoto kwenye baadhi ya shule ikiwamo Shule ya Msingi Kijenge, Sekondari ya Olorieni na kituo cha watoto yatima cha Moses Comfort cha USA River Arusha.

Lakini, pamoja na kuwafikia walio shuleni hajawasahau wanaoishi kwenye mazingira magumu hasa wanaokaa mitaani. Ameanzisha program maalumu za kuwaagusa za ‘TechAkid na TechAkidToCode akiwafundisha masuala ya kimaisha, teknolojia za kielektroniki, vifaa vyake ili wazitumie ziwasaidie, maarifa na stadi mbalimbali kuwakwamua na kuwawezesha kuzisaidia pia jamii zao.

 Mbwambo anapozungumza na Nipashe anaeleza kuwa anatumia nguvu, mali na juhudi binafsi, vifaa, fedha  na michango ya wadau mbalimbali kufanikisha mikakati hayo na  mafunzo kwa watoto anaoamini ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya nchi.

“ Mpaka sasa tumewafikia watoto zaidi ya 500. Lengo la Gentech nikuwahudumia watoto masikini wasio na uwezo wa kupata elimu wala vifaa vya kiteknolojia ili kupunguza pengo la kidijitali kati ya watoto wa familia za wenye nacho na wasio nacho.” Anasema Mbwambo.

 Anaeleza kuwa hayuko peke yake anashirikiana na Adam Malick mwanzilishi mwenza wa taasisi ya Gentech. Akiwa mtaalamu wa TEHAMA na kwamba ni  mshiriki  muhimu kwenye kutimiza azma hiyo, akiandaa mitaala, na vifaa sahihi vya kujifunzia na kufundishia pamoja na kuwa na matumizi chanya na yenye tija ya teknolojia kwa watoto hao.

 Mbwambo anawakilisha matumaini na ujasiri kwa vizazi vijavyo, mtu  anayeweza kuitwa kijana wa mfano wa kuigwa na kielelezo cha mabadiliko katika jamii anayewafundisha vijana kujitoa kwa ajili ya wengine kwa manufaa ya taifa letu.

  MAISHA NI KUJARIBU

 “Mwaka 2020 niligombea ubunge jimbo la Same Magharibi kutokana na mazingira ya kisiasa wakati ule, nilifukuzwa chuoni, familia yangu ilikata tamaa na waliacha kutoa msaada. Nilibakia mwenyewe na "imani" yangu ya  kumcha Mungu, kumpenda jirani na jitihada binafsi nilisimama. Sikuwa na fedha wala marafiki wakunisaidia katika maono yangu ila niliona kuwa ni lazima kujaribu na huko ndiko kuweza.”

Anasema alipata nafasi ya kwenda Misri lakini fedha ikawa kikwazo kikuu.“Safari yangu ya masomoni Misri nilikwenda kwa msaada wa kanisa. Nauli nililipiwa na Mchungaji kanisani, Pastor Orche Mgonja wa kanisa la Lift Him up. Alinikopesha Shilingi million 1.5 ili nihudhurie mafunzo ya uongozi chini humo. 

Nilipofika kule nilikutana na viongozi mbalimbali, akiwemo Balozi wa Tanzania Misri wakati huo Dk.Emmanuel Nchimbi.”

Alikwenda kujifunza mafunzo ya uongozi chini ya Programu ya Rais wa Misri, Abdel Fatah El-Sis, na kutunukiwa cheti na nishani ya heshima. Alipewa pia fursa ya kutembelea Bunge Misri, Chuo cha Polisi (Accademy), alizuru mfereji wa Suez (suez Canal), mji mkongwe wa Alexandria na Makumbusho ya Taifa kujifunza zaidi kuhusu historia ya kiungozi tangu kale mpaka sasa.

Mbwambo anamtaja Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, kuwa ana nafasi katika maisha yake na amechangia kupata mafanikio, akieleza alivyomsaidia akiwa nchini Misri kwenye masomo

 “Baada ya mafunzo mimi na mwenzangu mmoja tukijijua hali zetu, tulishauriana tuutafute Ubalozi wa Tanzania tupate hifadhi siku mbili. Cha ajabu hata hatujafanya hivyo Balozi Dk. Nchimbi akatualika nyumbani kwake na tukakaa kwa siku mbili, alitupa fedha ili tununue zawadi, alitoa gari la ubalozi lituhudumie na asubuhi siku ya safari tulipelekwa uwanja wa ndege kwa heshima. Matendo hayo yote kwangu yalikuwa ushuhuda wa imani yangu na namna Mungu anavyoweza kuinua watu wakunisaidia katika mambo mbalimbali.”

 Balozi Nchimbi sikumfahamu kabla, sikuwahi hata kumuona lakini Mungu alimuinua akanitendea yote haya. Nami naamini nina deni la kuwatendea wengine mema kwa kuwapa elimu kama ambavyo mimi nimeshikwa mkono na wengine, anaeleza kijana huyo.

 TUSIKWEPE SIASA 

Mbwambo anaamini kuwa siasa si jambo la kukwepa. Ni kila kitu ndiyo inayoanzisha na kutunga sheria zote akimaanisha kazi za wabunge Dodoma  na wawakilishi visiwani Zanzibar. Kwa kuthibitisha hilo anasema ndiyo maana ni mwanachama wa CHADEMA, tangu mwaka 2008, na katika uchaguzi mkuu wa 2020 aligombea ubunge jimboni Same Magharibi.

Ingawa hakufanikiwa katika kura za maoni, anaeleza kuwa alimuunga mkono mgombea wa chama hicho Gervas Mgonja, na kuwa meneja wa kampeni yake.

Anawahimiza vijana kuacha mijadala ya kandanda na kukaa vijiweni bali waangalie maendeleo na kupenda kujiingiza kwenye masuala ya ubunifu, kujituma , uongozi, mijadala na kuibua fikra tunduizi (critical thinking) ili kupata mawazo yanayobadili maisha yao.