Wadau wanapofikiria ubatizo wa `2’ Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:03 PM Apr 23 2024
Mwami Tereza Ntare enzi za uhai wake.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwami Tereza Ntare enzi za uhai wake.

TEREZA Joseph Ntare aliyezaliwa 1927 na kufariki 1990, maarufu kama Mwami Tereza Ntare II ni mwanamama nguli, aliyefanya makubwa kwa taifa hili, lakini wengi hawamfahamu.

Aidha, alikuwa mhifadhi mkuu wa jamii, mila na desturi, uongozi bora na mpiganaji, Chifu Mkuu mwanamke wa kwanza akiongoza machifu wote wa Tanganyika wakati wa ukoloni wa Muingereza.

Akitajwa kuwa mwanamama aliyeruka viunzi na kuukabili mfumo dume na ukosefu wa usawa wa kijinsia, akipaa kama ‘tai, kuleta mawindo ya  ushindi kwenye majukumu yote aliyokuwa akiyasimamia, inasikitisha kuwa  hafahamiki na wengi.

Kwa kuona upungufu huo, Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake kwa kushirikiana na Mtandao wa Ke-Storia, Makumbusho ya Taifa na familia ya Mwami Tereza , unaandaa jukwaa la kusherehekea mafanikio yake.  

Mengi yanazungumzwa kwenye maadhimisho yake, yanayofanyika kwenye Makumbusho ya Taifa Dar es Salaam mapema mwezi huu.

Anasifiwa kwa jinsi alivyofanikisha kupatikana uhuru mwaka 1961, kando na hilo ujasiri, kuwa na fikra zilizopevuka, kuona mbali na kutambua vipaumbele kunampa heshima ya kuwa mama aliyeota na kuitimiza ndoto ya kuanzishwa Chuo Kikuu –UDSM.

Ni maelezo ya meja mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Minaeli-Hosana Mdundo, anayeieleza hadhara ya washiriki wa mafanikio ya Mwami Tereza yakihusisha wanafamilia, asasi za kiraia, watendaji wa serikali.

“Katika Mkutano Mkuu wa TANU uliofanyika Tabora mwaka 1958 pamoja na ajenda mbalimbali, mojawapo ni ujenzi wa chuo kikuu cha Tanganyika.

Mwami Tereza, alikuwa mjumbe wa mkutano huo na akawa miongoni mwa waliopewa jukumu la kufanikisha kujengwa chuo hicho.” Anasema Minaeli.

Anaongoza: “Mwami Tereza akatoa wazo kuwa majengo ya chama yaliyoko ofisi ya CCM Mtaa wa Lumumba Dar es Salaam, yatumike kuanzisha chuo kuu cha Tanganyika. Akamsindikiza Kamanda wa Vijana Rajabu Diwani (marehemu) kufikisha wazo kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere naye akaafiki.”   

Minaeli mtunza nyaraka za zamani (archivist) mstaafu, anatoa ushuhuda huo na kueleza kuwa chuo kikuu cha UDSM kilianza miezi michache kabla ya uhuru na Mwami Tereza ni mbeba maono.

Katika kusanyiko hilo wengi wakatafakari jinsi mwanamama huyu alivyoshiriki kuanzisha UDSM na kuhoji hivi hakikustahili kupewa jina Lake?

Moja ya mabweni katika chuo hicho yana jina la Dag Hammarskjöld, (Hamaskod) Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, aliyeuawa 1961 katika ajali ya hekopta akiwa kwenye misheni ya kusaka amani ya Congo.

Ni ujumbe kwa serikali kumuenzi mwanamama huyo mashuhuri, shujaa na aliyekuwa na bidii ya kujenga Tanzania yenye maisha bora kwa kila mmoja kwa kuiita UDSM Chuo Kikuu cha Mwami Tereza Ntare II.

KUWASAHAU KINAMAMA

Maadhimisho ya mafanikio ya Mwami Tereza, yanagundua kuwa wanawake wamefanya mengi lakini hawaonekani katika uandishi wa historia.

Profesa Ruth Meena, kutoka Mtandao wa KE-Storia, (Her Story), unaotetea haki za wanawake, kuziibua na kuziandika upya kwa usahihi kwa kuonyesha mafanikio, anasema licha ya Mwami Tereza kufanya  makubwa historia yake haifahamiki tena inasahaulika.

Anasisitiza kuandika na kuweka uwiano sawia (balanced story) ya wote waliochangia maendeleo na mafanikio ya Tanzania.

Anaongeza kuwa ni wakati wa kuachana na mtindo wa kuandika taarifa zinazoonyesha upande mmoja na kuupuza mwingine hasa wa wanawake.

Anashauri kurekebisha historia, kumbukumbu na taarifa zote zilizoandikwa kwa upendeleo wa upande mmoja na kubagua kundi jingine ambalo pia limechangia mafanikio ya taifa katika nafasi mbalimbali.

“Jukumu la kurekebisha kumbukumbu na taarifa hizo au kuzikomboa upya zilizopotoshwa lisiachiwe familia bali serikali iongoze masahihisho ya mambo yote yaliyowaondoa wanawake katika mapambano ya ukombozi wa taifa,”anasema Profesa Ruth.

Anaongeza zaidi: “Vitu vyote vilivyoporwa na wakoloni hasa vichwa vya wapigania uhuru wawe wanawake au wanaume, serikali isimamie kuvidai na kuvirudisha isiziachie familia kuvidai.”

Akizungumza mbele ya Waziri wa Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro, Prof Ruth, anasema inashangaza Makumbusho ya Taifa kwa miaka mingi haikuwa na picha ya mwanamke na kusema ni wakati wa kufanya mabadiliko.

Anasema ni mambo yaliyoanzishwa na kupotoshwa na wakoloni lakini wakati umefika yasahihishwe ili kuweka uwiano sawa wa wanawake na wanaume waliochangia kufikisha Tanzania hapa ilipo leo.  

MAKUMBUSHO KIGOMA
 Waziri Ndumbaro, akizungumza katika maadhimisho hayo, anaahidi serikali itajenga Makumbusho ya Mwami Tereza Kigoma kuenzi kazi zake na michango mbalimbali ya wanawake walioshiriki katika harakati za ukombozi na maendeleo ya Tanzania.

 Anasema makumbusho ya Mwami Tereza yatahifadhi historia sahihi itakayokuwa imeandikwa na Watanzania wenyewe.

Anatangaza kuwa kuanzia sasa kila Machi 8 Siku ya Wanawake Duniani, itakuwa siku ya kuadhimisha na kumuenzi Mwami Tereza Ntare II.

Agnes Shinganya mjukuu wa Mwami Tereza, akizungumza kwa niaba ya familia anasema ni dhamira ya muda mrefu ya familia ya Mwami kumuenzi kiongozi huyo baada ya kuona historia yake, inasahaulika na inapotoshwa.

Anasema wameazimia kuanzisha Makumbusho ya Mwami mkoani Kigoma ili kuendelea kuhifadhi historia ya kiongozi huyo wa jamii wa watu wa eneo la Heru juu, aliokuwa anawaongoza.

Anaamini Makumbusho hayo ni chanzo cha mafanikio kiutafiti, utalii na kuchangia maendeleo ya elimu.

KURUDISHA FUVU ZA ZINJI

Joseph Macha, Kaimu Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa na Nyumba ya Utamaduni, anasema taasisi hiyo inamuenzi Mwami Tereza kwa  mambo makubwa aliyolifanyia taifa ikiwamo kurudisha fuvu la binadamu wa kale   Zinjanthropus kutoka Ulaya, akiwa mjumbe wa bodi.

Fuvu hilo ni la binadamu wa kwanza lilinalokadiriwa kuwa na umri wa miaka milioni 1.75 iliyopita lililogunduliwa mwaka 1959 na wanaakiolojia Mary na Louis Leakey katika Bonde la Olduvai Gorge mkoani Arusha.

Macha anaongeza kuwa makumbusho hiyo imekusanya na kuweka taarifa za historia ya Mwami Tereza  na kwamba yapo  mengi anayokumbukwa kuyasimamia kwa mafanikio.

“Amekuwa chifu kiongozi wa machifu wote Tanzania ,Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii , mjumbe wa bodi ya Makumbusho ya Taifa.

Anaahidi kushirikiana na wadau mbalimbali katika kufanya utafiti na kukusanya kumbukumbu zitakazofanikisha kuanzishwa Makumbusho ya Mwami Tereza kuenzi historia na mafanikio aliyoliachia taifa.