Bashe aanika walivyonasa madudu ushirika

By Vitus Audax , Nipashe Jumapili
Published at 11:53 AM May 05 2024
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.
PICHA: MAKTABA
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe, aeleza mchezo mchafu unaofanywa na vyama vya ushirika katika minada ya uuzaji wa mazao kwa kufanya udalali katika bei za wanunuzi na kusababisha wakulima kuendelea kuumizwa.

Bashe ameeleza hayo bungeni wakati akijibu hoja mbalimbali za wabung, ikiwamo ya kuitaka serikali kuweka bei elekezi ya ununuzi wa mazao hususani mahindi, korosho na kahawa yanayouzwa bei ya chini pamoja na kuuzwa tofauti katika maeneo mbalimbali nchini.

Akijibu hoja hizo, Waziri Bashe amesema si kwamba mazao yanauzwa bei ya chini, bali hali hiyo inasababishwa na watu wachache kuyafanyia udalali na kupata fedha nyingi tofauti na anayopewa mkulima sokoni.

Bashe amesema hujuma hizo kufanywa na vyama vya ushirika na kutaja Katheri akitoa ushahidi bungeni wa karatasi mbili kuwa ni sehemu ya fomu za ununuzi za kampuni ya Harmone Agro Ltd kuwa zinawekwa kwenye debe la mnada na moja ikiandikwa bei na nyingine haina.

Amesema ikifika usiku, ufunguo mmoja anakuwa nao ofisa ushirika na mwingine kiongozi wa ushirika ambao wanaitana na kufungua sanduku  na wakishamaliza wanampigia mnunuzi na kumlaghai.

“Wanasema fulani kaandika Sh. 2,000 na wewe umeandika Sh. 1,980 unaonaje uandike Sh. 2,010, alafu sisi utatupa Sh. 30. Kwa hili nina ushahidi, Bunge likiwa tayari nitaweka video ambazo tumerekodi vikao vya siri,” amesema huku Bunge likionyeshwa video hiyo ikionyesha watu watatu wakijadili jambo.

“Kinachofanyika kwa kuwa tumeshakubaliana tunaitoa ile karatasi ya bei halali aliyoandika inawekwa bei waliyokubaliana saa nane usiku alafu wanapeana Sh. 30 au Sh. 50,” amesema.

Amesema hilo walilibaini kupitia uchunguzi uliofanywa na kamati aliyounda na kufanya kazi kwa kipindi cha miezi mitatu ambapo walikutana na upinzani mkubwa katika ngazi za wilaya.

“Na mimi nilijua kwa kuwa kuna ajali za kisiasa niliwaambia kila mnapofanya mkutano hakikisheni mnarekodi kwa siri na kwa dhahiri, ambapo tulibaini wastani wa fedha iliyochukuliwa na watu wa Katheri  ni  Sh. 40 hadi Sh. 60, sawa na zaidi ya Sh. bilioni 20 wamegawana,” amesema.

Waziri Bashe amesema serikali haiwezi kuruhusu hujuma hiyo na kutoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe kwa ushirikiano wake wa kuzuia mnada wa ufuta uliotakiwa ufanyike siku tatu zilizopita, ambako walikuwa wamekubaliana debe liwekwe alafu lifunguliwe baada ya siku tatu ili kufanikisha hujuma hizo.

Amesema baada ya kubaini, alimwagiza Mkuu wa Mkoa pamoja na Mkuu wa Wilaya kuzuia kwa kuwa wakulima si wajinga, wanafahamu bei ikishuka na pale inapopanda.

Pia amesema kutokana na hali hiyo walianza mikutano ukiwamo wake na Waziri Mkuu uliofanyika wilayani Karagwe, ambako walikuta kahawa inauzwa kwa Sh. 700 lakini baada ya mkutano huo, inauzwa Sh.3,000.

“Tatizo si mfumo wa ushirika, tatizo ni ili kiongozi wa ushirika aibe ni lazima ofisa ushirika wa wilaya ashiriki kwenye wizi huo, tutazidi kuwabaini wahujumu hao na serikali itaweka mfumo maalumu wa kubaini bei elekezi,” amesema.

Amesema utaratibu huo utaanza na zao la ufuta, mbaazi na korosho na kuwapa haki ya kukataa bei inayoshindaniwa na wanunuzi.

RIPOTI YA CAG

Licha ya hujuma hizo, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2022/23 imebaini kuwa Mamlaka 20 za serikali za mitaa hazijakusanya jumla ya Sh. bilioni 5.22 katika chanzo kinachohusu ushuru wa mazao.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kushindwa kukusanya mapato husika ni kinyume na kifungu cha 7(1) (g) cha Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290 inayotaka malipo ya ushuru wa mazao kwa mnunuzi kutozwa asilimia tatu ya bei ya lango la shamba katika mazao ya biashara.

RC ADAKA VIGOGO

Waziri Bashe amemshukuru na kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, kwa kuwakamata na kuwaweka ndani maofisa ushirika watatu wa halmashauri, watendaji pamoja na madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa tuhuma za kujihusisha na hujuma za aina hiyo katika zao la tumbaku.

Amesema watu hao walikamatwa kwa kufanya ukangomba (hujuma) katika zao hilo na kudai kuwa, amebaki Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora ambaye amedai kuwa, aliiba mbolea za wakulima na sasa yupo mtaani.

Amesema Meya huyo hana kinga ya kushtakiwa na kuagiza yeyote atayehujumu juhudi za serikali, achukuliwe hatua stahiki bila kujali wadhifa wake, wala ukaribu wake na kiongozi yeyote.

“Niwape moyo wakuu wa mikoa pamoja na wakuu wa wilaya, kuwa yeyote anayehujumu shughuli na miradi ya wakulima katika ngazi ya Wilaya nchini mna mamlaka mliyopewa na Rais, itumieni maana hatutaruhusu nguvu zinazopelekwa na serikali alafu watu wachache wakafaidike na jasho la wakulima,” amesema.

UTITIRI TOZO

Waziri Bashe ametumia Bunge hilo kupiga marufuku utitiri wa tozo kwa wakulima tofauti na zile zilizowekwa kwa mujibu wa sheria zikiwamo tozo za Sh. 20 kwa kata,20 kwa wilaya pamoja na Sh. 10 kwa mkoa, na kuwa tozo zitakazobaki ni zile zinazotambuliwa na serikali.

“Fedha hizo zote ukipiga hesabu kwa tani 300,000 ni sawa na Sh. bilioni 50 mkulima anachukuliwa, hivyo halmashauri ikishachukua ushuru wake unatosha,”amesisitiza.

Amesema fedha hizo zilikuwa zinakatwa kwa madai ya ujenzi wa maeneo husika na kueleza kuwa kwa sasa serikali inapeleka fedha moja kwa moja katika maeneo husika, hivyo hakuna haja ya kuwanyonya wakuli.

Vilevile amesema serikali itapunga Sh. 10 kutoka kwenye tozo ya bodi ya korosho na Sh.10 kwenye tozo ya tari, ili kuondoa mzigo mkubwa kwa wakulima.