Bilioni 3.6 kufungua miradi nane Same

By Ashton Balaigwa , Nipashe Jumapili
Published at 04:50 PM Apr 07 2024
Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni.
PICHA: MAKTABA
Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni.

MKUU wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni amesema jumla ya miradi nane ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 3.6 inatarajiwa kupitiwa na mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024 ikiwemo ya barabara, vijana, elimu, maji, afya pamoja na mazingira.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema hayo wakati akitoa taarifa ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024 ambao utapokelewa kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Njoro asubuhi ya Aprili 08 ukiwa wilayani Mwanga.

Aidha, Kasilda amesema baada ya kuupokea Mwenge utakimbizwa wilayani humo Km 138.4 katika mbio hizo miradi minne itafunguliwa, mitatu itatembelewa na mmoja utawekewa jiwe la msingi ambao ni mradi wa kwanza wa barabara uliopo same mjini.

“Niwaombe wananchi wote ambao wapo wilayani Same wahakikishe wanajitokeza kwa wingi shuleni hapo ili kuupokea Mwenge huo kwa shamra shamra, nderemo na vifijo lakini pia kujitokeza kwa wingi kwenye mkesha wake pale uwanja wa Shule ya Msingi Hedaru.”

Pia amesema kuwa maandalizi muhimu ya kuupokea Mwenge huo tayari yamekamilika ikiwemo miradi ya maendeleo itakayopitiwa lakini pia jukwaa la viongozi pamoja na la wasanii kwenye eneo la mkesha wa Mwenge ambapo imepangwa kufanyika viwanja vya Shule ya Msingi Hedaru.

Nao baadhi ya viongozi wa madhehebu dini Wilayani humo wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti wamesema kuwa wananchi wanapaswa kutambua kufika kwa mwenge Wilayani humo ni moja ya sehemu ya maendeleo kwao kwani miradi mbali mbali ya maendeleo itafunguliwa hivyo hawanabudi kujitokeza kwa wingi kusikiliza maelekezo muhimu kutoka kwa viongozi wa mbio za Mwenge kitaifa.

Mwaka 2024 mbio za Mwenge wa Uhuru zimebeba kaulimbiu isemayo “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu”.