DC akemea watendaji kuwatosa wananchi

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 05:20 PM Apr 14 2024
MKUU wa Wilaya ya Muheza mkoani  Tanga, Zainabu Abdallah.
PICHA: MAKTABA
MKUU wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Zainabu Abdallah.

MKUU wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Zainabu Abdallah, amekemea tabia ya watendaji wa serikali kukaa ofisini badala ya kwenda kwa wananchi kutatua kero zinazowakabili.

Amesema watendaji hao wanapaswa kubadilika na kutekeleza kwa vitendo majukumu yao kwa kuwafuata wananchi waliko na kusikiliza kero zikiwamo migogoro ya ardhi.

Abdallah amesema hayo wakati akisikiliza kero za wananchi katika uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti wilayani hapa ijulikanayo ‘Soma na Mti’ iliyofanyika katika Shule za sekondari za Potwe na Kwabastola  kata ya Makole. Takribani miti  4,000 ilipandwa kupitia kampeni hiyo.  

Watendaji  wa serikali, amesema lazima waende kwa wananchi kusikiliza kero ikiwamo migogoro ya ardhi na kuzitatua badala ya kumsubiri mkuu wa wilaya aende kwa  wananchi. 

Amesema mtendaji yeyote wa serikali katika idara yake ambaye atashindwa kwenda kusilikiliza malalamiko ya wananchi na kuyatatua basi ahame katika wilaya hiyo.

"Wewe mtendaji ni lazime utoke uende kwenye maeneo ukaangalie ni jinsi gani unaweza kusuluhisha migogoro ya jamii na wawekezaji,” amesema.

Pia amesema dhamira ya serikali ni kuleta wawekezaji nchini waishi vizuri na wananchi wa wilaya yaa Muheza na si kuanzisha migogoro ya ardhi. 

"Rais Samia (Suluhu Hassan) ameifungua nchi kwa uwekezaji, amekwenda nchi mbalimbali duniani kutangaza fursa za uwekezaji tulizo nazo hapa nchini na amewaita wawekezaji wamekuja nchini kuwekeza. Sasa  kukiwa na migogoro na wananchi, itakwamisha juhudi za Rais," amesema.

“Wawekezaji tunawapenda waje kuwekeza nchini lakini nao wananchi wana nafasi yao. Wanalima mashamba, wanapanda mazao yao ili kusomesha Watoto. Sasa mkiwafukuza kwa ajili ya kumpa mwekezaji ardhi ndio inaleta migogoro. Hiyo sitaki katika wilaya hii,” amesema. 

Amesema baadhi ya watendaji wa serikali katika halmashauri wanatoa ardhi ya wananchi kwa wawekezaji kwa maslahi yao na kusababisha migogoro mikubwa kitu ambacho si kizuri. 

Mkuu wa wilaya ameema wiki iliyopita alikwenda katika kijiji cha Kambai, kata ya Kwezitu, ambako kumetokea mgogoro wa ardhi ya mashamba kati ya wanachi na mwekezaji, hivyo kusababisha kutokea fujo jambo ambalo si zuri.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa wilaya  amewataka vijana kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Ameliwahamasisha vijana na wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo ili kuleta mabadiliko katika jamii.

Nichukue nafasi hii kuwahamasisha mama zangu, dada zangu pamoja na vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa pindi mchakato utakapotangazwa rasmi," amesema.