Mabaraza ya ardhi kwenda mahakama

By Augusta Njoji , Nipashe Jumapili
Published at 04:37 PM May 05 2024
Waziri wa Wizara hiyo, Jerry Silaa.
PICHA: MAKTABA
Waziri wa Wizara hiyo, Jerry Silaa.

SERIKALI imeandaa mapendekezo ya kuhamisha shughuli zinazofanywa na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwenda mahakama.

Waziri wa Wizara hiyo, Jerry Silaa, ameyasema hayo bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Rorya (CCM), Jafari Chege.

Katika swali lake, Mbunge huyo alihoji lini serikali itahamisha mabaraza hayo  kwenda kwenye mfumo wa mahakama.

Silaa akijibu swali hilo, amesema katika jitihada za kuboresha mfumo uliopo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi nchini, serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeandaa mapendekezo hayo.

Katika swali la nyongeza, Mbunge huyo amesema Wilaya ya Rorya haina baraza la ardhi hali inayosababisha wananchi kusafiri umbali wa kilomita 60 hadi 100 kwenda Tarime kufuata huduma hiyo.

“Umbali huu unasababisha wananchi kukata tamaa kushughulikia haki zao za kimsingi za kisheria za utatuzi wa migogoro ya ardhi, je, serikali haioni haja ya kuanzisha baraza la ardhi Rorya,”amesema.

Amesema pia, kumekuwapo na kukithiri kwa vitendo vya rushwa kwenye mabaraza hayo na kuhoji mpango mkakati wa serikali wa kukomesha vitendo hivyo vinavyowanyima haki wananchi.

Waziri Silaa akijibu swali hilo, amesema kwasasa nia ya serikali ni kuondosha mabaraza hayo na kuyapeleka mahakama kutokana na mifumo ya utoaji haki kuboreshwa.

“Nikiri kumekuwa na malalamiko mengi ya tuhuma za rushwa kwenye mabaraza haya, wizara itakapopata taarifa mahsusi za baraza ambalo limefanya maamuzi ya shauri kwa kushawishiwa na rushwa tutachukua hatua,”amesema.

Hata hivyo, amesema wakati mchakato huo unaendelea wa kuhamisha mabaraza kwenye mahakama, kuna wilaya 36 hazina mabaraza na watakapopatikana wenyeviti mabaraza hayo yataanzishwa.