Mbinu ya kukomesha mikopo kausha damu

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 09:38 AM May 26 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, John Wanga.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, John Wanga.

USHIRIKIANO wa wananchi na viongozi wa serikali ndiyo njia pekee itakayowezesha kuwafichua wamiliki wa taasisi za ukopeshaji fedha zisizo rasmi ili watakaobainika hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Hayo yalisemwa juzi na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, John Wanga, alipokutana na timu ya wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo inaendelea kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa mkoa wa Kagera katika wilaya za Bukoba, Missenyi, Muleba na Biharamulo. 

“Sisi kama viongozi wa serikali tunatakiwa tuendelee kushirikiana na Wananchi kuwakemea watoa huduma wasio na nia njema kwa taifa wanaojali maslahi yao binafsi”, alisema Wanga. 

Alisema serikali haitasita kuwachukulia hatua watu wote watakaobainika kwenda kinyume cha maelekezo waliyopewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kabla hawajapatiwa leseni za kuendesha shughuli za utoaji mikopo. 

Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Flavian Nturwa, alisema ni wajibu wa waratibu wote wa huduma ndogo za fedha kutoa elimu kwa wananchi katika ngazi zote ili wawe na uelewa mpana wa masuala ya fedha. 

“Tutahakikisha tunafanya mikutano ya mara kwa mara kwa wananchi wa pande zote, watoa mikopo na wapokeaji ili wawe na uelewa wa pamoja hususan elimu ya mikataba ili kuepuka kusaini mikataba yenye masharti magumu”, alisema Nturwa. 

Naye mtoa huduma za mikopo, Salehe Hamisi, alisema elimu itolewe kuhusu utaratibu wa kusajili taasisi za fedha ili Wafanyabiashara waweze kujisajili kwa wingi na kutambulika rasmi. 

Ofisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Mary Mihigo, aliwasisitiza wananchi kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha na kutunza akiba. 

Wizara ya Fedha inaendelea na utoaji elimu kwa wananchi kuhusu huduma ndogo za fedha ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na elimu ya huduma ndogo za fedha.