Mbunge ataka umiliki wa ndege uwe chini ya ATCL

By Vitus Audax , Nipashe Jumapili
Published at 12:28 PM Apr 21 2024
MBUNGE wa Jimbo la Mlalo (CCM), Rashid Shangazi.
PICHA: MAKTABA
MBUNGE wa Jimbo la Mlalo (CCM), Rashid Shangazi.

MBUNGE wa Jimbo la Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, (CCM) ameitaka serikali kuondoa umiliki wa ndege katika Wakala wa Ndege za Serikali Tanzania (TGFA) na kuwekwa chini ya usimamizi wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ili kuondoa utaratibu wa serikali kujikodishia mali zake yenyewe na kushindwa kulipa.

Shangazi ametoa kauli hiyo wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nchi – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka 2024/25.

Amesema hatua ya TGFA kulikodisha ATCL ndege ambazo zinasomeka kama mali za serikali moja kwa moja, licha ya serikali kuingia kwenye madeni makubwa ya yenyewe kwa yenyewe, pia imekuwa ikisababisha ndege hizo kukamatwa nje na wadai wa serikali.

“Sasa unapokodisha ndege imenunuliwa na serikali kwa shirika la serikali. Hapa cha kutazama ni kuwa ndege ya serikali inapokuwa kwenye wakala wa serikali deni linakuwa ni la serikali, hali inayofanya ndege hizo zikamatwe.

“Tumeishakamatiwa ndege hapa hivi karibuni na nyinyi ni mashahidi kwa sababu, ndege zinasoma kuwa ni mali ya serikali, lakini zingekuwa za ATCL, ingekuwa siyo rahisi kuzikamata kwa kuwa, ni mali ya shirika, japo mwenye shirika hilo ni serikali,” amesema.

Shangazi amesema serikali inatakiwa kuliona hilo na kuchukua hatua za haraka ili kuepuka makandokando hayo ambayo nchi imekuwa ikiendelea kukutana nayo.

Naye, Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina, amesema taifa linatakiwa kutafakari upya mifumo ya dhana ya utawala bora, kwa kuwa kuna vitendo vinafanyika waziwazi vinavyoonesha uvunjaji wa Katiba wa moja kwa moja kwa moja pamoja na kutozingatia haki za binadamu.

Amesema ipo haja ya serikali kutafakari mifumo ya kiutawala, kwa kuwa hakuna mtu mkubwa wala mdogo, mgawanyo wa madaraka upo chini, hali inayosababisha malumbano ya viongozi kila mara na kushindwa kutenda kazi ipasavyo.

“Huko marumbano ni makubwa mara Ma-DC na wakurugezi. mkurugenzi na mbunge, wakuu wa mikoa, mawaziri na makatibu wakuu vivyo hivyo mwisho wa siku mifumo inaenda ovyo.

“Suala lingine ni la uteuzi wa viongozi pamoja na ajira bila kufuata taratibu za kiushindani hali inayosababisha kupata viongozi dhaifu, watendaji dhaifu wasioweza kufanya kazi zao kwa ufanisi hali inayosababisha kumpa kazi kubwa Rais Samia Suluhu Hassan kuteua mara kwa mara,” amesema.

Mpina amesema kwa sasa nafasi hizo za uteuzi zinatakiwa zishindanishwe ili kupata watu wenye ujuzi na ufanisi katika kazi, lengo ni kuondoa usumbufu kwa Rais kusoma wadhifa wa watu mara kwa mara na kudai kuwa, hata hivyo anaowachagua wamekuwa wakimkwamisha katika kazi zao.

Amemtaka waziri kuja na suluhisho la suala liloibuliwa kuhusu watu wasio watanzania kupewa vyeo pamoja na ajira nchini, akihoji kuwa ni kwa nini waziri hakuliona hilo kama changamoto katika sekta hiyo.

“Tupate majibu ya hao, waliotajwa kuajiriwa ikiwa siyo raia wa Tanzania, ni kina nani? Na kwa nini wanaendelea kuwa watumishi bila kuwa na uhalali wa kufanya kazi nchini,” amehoji Mpina.