TADB yaikabidhi serikali gawio la Sh.mil 850

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 03:23 PM May 26 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) Frank Nyabundege akizungumza na wanahabari.
Picha: Maulid Mmbaga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) Frank Nyabundege akizungumza na wanahabari.

MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Frank Nyabundege, amebainisha kuwa benki hiyo imetoa gawio la Sh. milioni 850 kama sehemu ya faida waliyoipata kwenda serikalini ikiwa ni asilimia sita ya faida waliyoipata kwa mwaka.

Aliyabainisha hayo leo mkoani Dar es Salaam, pembeni ya kikao cha mwaka 'annual meeting' kilichowakutaniswa wajumbe wa bodi, menejimenti na msajili wa hadhina, kwa lengo la kujadili utendaji wa benki hiyo kwa mwaka 2023.

Amesema wanafurahi kuona benki hiyo inaendelea kukuwa kwa asilimia kubwa, na kwamba mwaka 2023 mtaji wake uliongezeka kutoka Sh. Bilioni 448 hadi 607, na kutengeneza faida ya kabla ya kodi yaani faida ghafi takribani Sh. Bilioni 19.

"Mwaka huu serikali imeipatia TADB Sh. Bilioni 170 kwa lengo la kuiongezea mtaji, jambo linaloisaidia kuendelea kukuwa na kuzidi kuwafikia wananchi wengi hasa wakulima wafugaji na wavuvi," amesema Nyabundege.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurungezi TADB, Ishmael Kasekwa,  ameihakikishia serikali ambayo ndio mwanahisa mkuu, kwamba wao kama bodi wataendelea kuisinania benki hiyo ili kufanya vizuri katika utendaji na kitimiza malengo ambayo serikali ilikusudia ilipoianzisha.

Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu, amesema benki hiyo ilianzishwa kimkakati na mpaka sasa serikali imewekeza mtaji  wa takribani Sh. Bilioni 315 ili kuwaendeleza wakulima.

Amesema watu wengi wanachukulia kwamba kilimo ni sehemu yenye 'risk' kubwa lakini kwa sasa ni tofauti na wanavyofikiria kwasababu benki hiyo kwa mwaka huu imezalisha faida ya Sh. Bilioni 14, huku akiwapongeza wanufaika wote ambao wamekuwa wakikopa na kurejesha fedha zao.

"Pia niwashukuru bodi, menejimenti pamoja na wafanyakazi wote kwakuwa wameendelea kuhakikisha kwamba uwekezaji wa serikali unaendelea kuimarika na hauyumbi na tunazidi kuwa na benki ambayo itakuwa na kuwafikia watu wengi hasa wakulima," amesema Mchechu.

Hata hivyo, amebaibisha kuwa mwaka ujao wa fedha wanategemea kama mabo yataenda vizuri benki hiyo itaongezewa zaidi ya Sh. Bilioni 100 kama mtaji, na kwamba wamewataka waweke sera ya urejeshwaji wa faida kwasababu serikali inataka iendelee kutoa huduma kwa wananchi kupitia mapato hayo.