Waziri aagiza uchunguzi ubadhirifu fedha vijiji mradi wa wanyamapori

By Munir Shemweta , Nipashe Jumapili
Published at 05:14 PM Apr 14 2024
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda.
PICHA: MAKTABA
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda.

MBUNGE wa Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda, amemwomba Mkuu wa Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, Alhaji Majid Mwanga, kuunda kamati ya kupitia mapato na matumizi ya fedha za Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) katika Halmashauri ya Mpimbwe ili kubaini kama kuna ubadhilifu ili wahusika wachukuliwe hatua.

Pia amemwomba mkuu huyo wa wilaya kuchunguza Sh. milioni 44 zilizotolewa na mkandarasi anayejenga barabara ya Kibaoni hadi Sitalike, zinazodaiwa kulipwa kwa kijiji bila kufuata utaratibu.

Pinda amesema hayo kwa kwa nyakati tofauti wakati wa mikutano yake ya hadhara na wananchi wa vijiji vya Mirumba, Ilalangulu na Kibaoni katika Halmashauri ya Mpimbwe, wilayani hapa. 

Amesema hayo baada ya kubadilishwa uongozi wa WMA ndani ya mwezi mmoja tu ambapo kamati ilifanikiwa kukusanya Sh. milioni 200 tofauti na kamati iliyokaa kwa zaidi ya miaka 10 na kudaiwa kutosaidia maendeleo yoyote ya vijiji husika.

"Iundwe tume ya kupita kitabu kwa kitabu tujue miaka 20 fedha zetu zilienda wapi za wananchi hao. Wiki  mbili Sh. milioni 200, hebu tuwaulize miaka 20 wameleta nini?" amehoji Pinda.

"Pia kuna ubadhilifu wa Sh. milioni 44 zilizotolewa na mkandarasi anayejenga barabara ya Kiabaoni- Sitalike ambaye amelipa kwa kijiji bila utaratibu. Uchunguzi nani amechukua fedha taslimu ambazo hazijulikani zilipokwenda wapi ufanyike," amesisitiza.

Pinda amesema mpango wa WMA una faida kubwa kwa vijjji vinavozunguka hifadhi na kutolea mfano wa wilaya ya Tanganyika inayonufaika. Kwa  mujibu wa Pinda, mwaka huu vijiji vinavyozunguka hifadhi vitapokea Sh. bilioni 16 .

Amesema kiasi chochote cha fedha kitakachopatikana kupitia WMA lazima wananchi wahusishwe matumizi yake ili fedha zinazokusanywa zitumike kwenye shughuli za maendeleo ya vijiji husika.

Alhaji Mwanga ameahidi kuunda haraka timu itakayohusisha vyombo vya ulinzi na usalama kama vile Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Polisi na Magereza ili kubaini kama kuna ubadhilifu wowote wa fedha za umma. Alisema iwapo itabainika hivyo, wahusika watachukuliwa hatua stahiki.

"Hakuna atakayepona katika suala hilo na lazima tutawashughulikia wahusika wote watakaobainika kuwaibia wananchi. Kazi hii tunaiweza na hatutacheka  na mtu hata mmoja,” amesema.

Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Jamii (WMA) katika Halmashauri ya Mpimbwe, wilayani ya Mlele, inahusisha vijiji vya Kibaoni, Mirumba, IIalangula na kijiji kimoja kutoka wilaya ya Nkasi.