W’biashara Soko la Coca-Cola walivyodhibiti uhalifu

By Mary Geofrey , Nipashe Jumapili
Published at 12:20 PM Apr 21 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Mtatiro Kitinkwi.
PICHA: MAKTABA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Mtatiro Kitinkwi.

WAMACHINGA wa soko la Coca-Cola Mwenge, Wilaya ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, wamefanikiwa kudhibiti makundi ya wahalifu waliokuwa wanajificha sokoni.

Makundi hayo ni wezi wanaovunja na kuiba katika nyumba za watu, wanaopora mali, wauzaji na wavutaji wa bangi, wanaojisaidia barabarani na wanaodhalilisha wanawake na wasichana kwa kuwatomasa bila ridhaa.

Katika taarifa ya Mwenyekiti wa soko hilo, Abdallah Samata, ameyoitoa kwa vyombo vya habari, imesema kutokana na kukithiri vitendo hivyo walilazimika kuchukua hatua za kufanya ulinzi shirikishi kuanzia mwezi Januari, mwaka huu.

“Sasa hivi ukipita soko la Coca-Cola Mwenge hutaamini unachokiona, ukiacha simu unaikuta, hakuna wavuta bangi, hakuna wanaopapasa wasichana au wanafunzi,” amesema Samata.

Aidha, amesema kabla ya kutangaza uamuzi huo walitoa taarifa katika Ofisi za Serikali ya Mtaa, kata na vituo vyote vya polisi kwa kupeleka barua ili kupata ridhaa hiyo.

“Viongozi wa serikali za mtaa, wilaya na Mkoa wa Dar es Salaam walitusikiliza na kuelewa nia yetu njema na kutuunga mkono katika kumaliza haya makundi. Walifika katika eneo letu la soko na kushuhudia hali halisi ya uharibifu, mmomonyoko wa maadili na uhalifu unaofanywa na baadhi ya watu,” amesema Samata.

Kadhalika, uongozi wa soko kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi walichukua hatua zinazoendelea ili kuliweka eneo la machinga pamoja na viunga vyake kuwa salama kwa wafanyabishara na watumiaji wote.

Kiongozi huyo amewasihi wafanyabiashara wa masoko mengine kuiga mfano huo kwa kuimarisha ulinzi na usalama wa maeneo yote ya biashara na kuondokana na dhana kuwa maeneo ya soko kutumika kuwa makazi ya wahalifu.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya Simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Mtatiro Kitinkwi, amesema operesheni hiyo imesaidia kumaliza wahalifu katika eneo hilo.

Amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano baina ya Jeshi la Polisi na wafanyabishara wa eneo hilo na kutoa rai kwa maeneo mengine kushirikiana ili kumaliza uhalifu na wahalifu katika mitaa na maeneo yao.