Zanzibar kufanya maonyesho ya Kimataifa ya utalii na uwekezaji Oktoba

By Beatrice Shayo , Nipashe Jumapili
Published at 07:40 PM Jun 09 2024
Zanzibar kufanya maonyesho ya Kimataifa ya utalii na uwekezaji Oktoba.
Picha: Beatrice Shayo
Zanzibar kufanya maonyesho ya Kimataifa ya utalii na uwekezaji Oktoba.

WAZIRI wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mudrick Ramadhan Soraga, ametangaza kufanyika kwa maonyesho ya Kimataifa ya utalii visiwani Zanzibar kuanzia Oktoba 25 hadi 26 mwaka huu.

Waziri  Soraga ameyasema hayo katika maonyesho ya Karibu Kili Fair (KKF) wakati akizindua rasmi msimu wa maonesho hayo yanayofahamika kama Zanzibar Tourism and Investment Show 2024.

Uzinduzi huo uliofanyika kwenye banda la Kamisheni ya Utalii Zanzibar kwenye viwanja vya Magereza Kisongo Mjini Arusha yanapofanyika maonyesho ya KKF.

Amesema kwenye maonyesho hayo kutatambulishwa fursa mbalimbali za kiutalii na uwekezaji uliopo kwenye sekta ya utalii Zanzibar na mazingira bora katika uwekezaji.

Aidha, amewaalika wadau wote wa utalii kushiriki kwenye maonyesho hayo makubwa na ya kihistoria yenye fursa mbalimbali.

Kufanyika kwa maonesho hayo ni muendelezo wa kuutangaza utalii na fursa zilizopo kwenye utalii  nchini ili kuchagiza na kuchochea tija ya kiuchumi na kijamii inayotokana na sekta ya utalii katika kuunga jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi.