ACT walia upigaji tril 3/- serikalini

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 10:13 AM Apr 21 2024
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu.
PICHA: ACT-WAZALENDO
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu.

CHAMA cha ACT Wazalendo kimechambua ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka 2022/23, kikitaka hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya watendaji wa serikali wanaonyooshewa kidole kufanya ubadhirifu wa jumla ya Sh. trilioni 3.14.

Dorothy Semu, Kiongozi wa ACT Wazalendo, wakati wa kuwasilisha uchambuzi huo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, amesema wamechagua maeneo 10 waliyoona ni muhimu zaidi Watanzania kuyatambua na wameyatolea mapendekezo ili yafanyiwe kazi, ikiwamo hoja hiyo ya ubadhirifu wa fedha za umma.

Amesema uchambuzi wao umebaini CAG ameibua hoja nyingi zinazopaswa kufanyiwa kazi. Baadhi ya hoja hizo zitazingatiwa kwenye uchambuzi wa bajeti wa kila wizara ya serikali utakaofanywa na wasemaji wao wa kisekta.

Waziri Kivuli wa Fedha, Mipango na Hifadhi ya Jamii wa chama hicho, Kizza Mayeye, amesema ripoti hiyo ya CAG imeendelea kuonesha uzembe unaofanywa na serikali uliosababisha upotevu wa makusanyo na mapato katika wizara, idara na taasisi za serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa, miradi ya maendeleo na mashirika ya umma.

Amesema wameona kwa mara nyingine vitendo au uamuzi wenye viashiria vya ubadhirifu wa fedha za umma katika utekelezaji miradi na majukumu mbalimbali ya wizara na taasisi za serikali kukiwa na hoja za ubadhirifu na upotevu wa fedha za makusanyo zenye jumla ya Sh. trilioni 3.14.

Amefafanua kuwa katika fedha hizo, halmashauri zimeonesha upotevu wa Sh. bilioni 167.8, wizara, idara na taasisi za serikali zina upotevu wenye thamani ya Sh. bilioni 103.32, gharama zinazotokana na ucheleweshaji kutelekezwa kwa miradi ya maendeleo zina jumla ya Sh. bilioni 744.1, dosari za kiusanifu za Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwenye miradi ya barabara sita Sh. bilioni 130.51, mradi wa BRT Sh. bilioni 28.05, Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere Sh. bilioni 327 na mashirika ya umma yana hoja zenye thamani ya Sh. trilioni 2.23.

"Taarifa ya CAG inathibitisha tena tatizo sugu la serikali kuendelea kupoteza na kutumia vibaya fedha za umma bila hatua za uwajibishaji kuchukuliwa. ACT Wazalendo tunataka watu wote waliohusika na ubadhirifu na uzembe uliopelekea upotevu wa fedha za umma wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria," Kizza amependekeza.

Waziri Kivuli huyo pia alizungumzia dosari ya fedha kutopitishwa Mfuko Mkuu wa Hazina, akiitaja ni mwanya wa ufisadi.

Amesema kuwa uchambuzi wao umebaini kuwa kwa mwaka 2022/23, jumla ya matumizi yenye thamani ya Sh. trilioni 3.2 yalifanywa bila kupita Mfuko Mkuu wa Serikali, sehemu kubwa ya fedha hizo inatokana na fedha zilizopelekwa moja kwa moja kwenye miradi kutoka kwa wadau wa maendeleo.

"Fedha hizi za miradi zinaonekana katika vitabu vya bajeti, lakini CAG hazioni kuingia Mfuko Mkuu na hivyo kutoka kwake ni kinyume cha sheria. Matumizi ya aina hii licha ya kuwa ni kinyume cha katiba na sheria za nchi, huwa ni kichaka cha kuficha ubadhirifu kwani kutumia fedha namna hii kunamnyima CAG kufanya kazi yake ya udhibiti wa fedha za umma," amehadharisha.

Waziri Kivuli huyo pia amesema CAG katika ripoti ya ufanisi wa usimamizi wa shughuli za kilimo, ameonesha wakulima wengi nchini hawajapata mbolea zenye ruzuku licha ya serikali kutenga wastani wa Sh. bilioni 150 kila mwaka.

Amesema CAG ameonesha kuwa wakulima milioni 2.55 kati ya milioni 3.4 waliosajiliwa katika mpango wa ruzuku (sawa na asilimia 75) hawakupata wala kutumia mbolea kupitia mpango wa ruzuku licha ya kuwa na sifa ya kupata mbolea hiyo ya ruzuku kwa mwaka huo wa ukaguzi.

UAGIZAJI PETROLI

Kizza pia amesema uchambuzi wao umegusa dosari katika uagizaji, uingizaji na usambazaji wa mafuta nchini, akiitaja ndiyo kiini cha kupanda kwa gharama ya mafuta nchini.

Amesema imebaini nchi haina Hifadhi ya Taifa ya Petroli, CAG akionesha kama Taifa kukosa hifadhi ya petroli ya mkakati kunaiweka nchi katika hatari ya kuwa na uhaba wa nishati wakati wa shida.

Vilevile amesema nchi ina uwezo mdogo wa miundombinu mafuta, CAG akionesha kuna bomba moja tu linalotumika kuingiza mafuta Tanga, Mtwara na Dar es Salaam na bomba hilo moja ndilo hutumika kusafirisha petroli na dizeli, baada ya kusafirisha petroli linasafishwa ili kupitishwa dizeli.

"Bomba hili limetumika kuanzia 2012 ambapo lilitumika kusafirishia Metric Tone 250,000, sasa linapitisha 650,000. Serikali ya CCM inafanya mchezo na suala hili nyeti, sisi tunaona ni lazima kuweka mkazo mkubwa sana kwenye eneo hili hasa ukizingatia mambo kadhaa yanaweza kuteteresha usambazaji wa mafuta duniani kama vile migogoro ya kieneo (vita Mashariki ya Kati), majanga, vikwazo vya kiuchumi kwa baadhi ya nchi," amesema.

DENI LA SERIKALI

Waziri Kivuli huyo pia amezungumzia hoja ya kasi ya ukuaji wa Deni la Serikali na hatari zake kwa taifa, akisema CAG ameonesha ukuaji wa kasi wa deni hilo. Hadi Juni 30, 2023, Deni la Serikali lilikuwa Sh. trilioni 82.25 sawa na Ongezeko Sh. trilioni 10. 94 (asilimia 15) kutoka mwaka wa fedha uliotangulia (2021/22).

"Uchambuzi wetu wa CAG kuhusu mwenendo wa Deni la Serikali ni kuwa kasi ya ukuaji wa Deni la Serikali inatishia maendeleo ya watu, uwezo wa nchi kujihudumia na kusababisha ukuaji wa uchumi unaoendeshwa na deni (debt driven growth)," amesema.

MIFUKO HIFADHI YA JAMII

Madai ya wafanyakazi Sh. bilioni 36.47 na michango yao (sh. bilioni 856.78 kutowasilishwa kwenye Mifuko ya hifadhi ya Jamii.

Kiongozi wa Chama hicho, Dorothy, amezungumzia hoja madai ya wafanyakazi Sh. bilioni 36.47 na michango yao Sh. bilioni 856.78 kutowasilishwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.

Amesema ripoti ya CAG kwa mwaka 2022/23 imeonesha madai ya Sh. bilioni 36.47 ya watumishi wa umma katika halmashauri 54. Madai hayo yanajumuisha malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi, stahiki za wastaafu na posho za kisheria.

"Kutokulipwa kwa madai haya kunaongeza ugumu wa maisha kwa wafanyakazi ikizingatia tayari gharama za bidhaa muhimu zinaendelea kupanda kila uchao. Pia ni kinyume cha kanuni ya utumishi wa umma inayoelekeza mfanyakazi yeyote wa serikali pale anapopandishwa daraja au kuteuliwa kwenye nafasi ya kiwango cha juu, alipwe malipo ya nyongeza ya mshahara yanayostahili.

"ACT Wazalendo tunaitaka na serikali na waajiri binafsi kuheshimu matakwa ya sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kuwasilisha kwa wakati michango ya wafanyakazi. Pia tunaitaka serikali kulipa malimbikizo ya madai yote ya watumishi na wastaafu," amesema.

MADUDU MWENDOKASI

Waziri Mkuu Kivuli na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Tanzania Bara, Isihaka Mchinjita amezungumzia hoja ya usimamizi mbovu wa mradi wa mabasi yaendayo haraka, maarufu mwendokasi.

Amesema CAG amebaini kuna usimamizi mbovu kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ambao upo chini ya OR-TAMISEMI. Mradi wa Sh. bilioni 217.48 wa kutoka Katikati ya Jiji hadi Mbagala umekamilika kwa asilimia 98.86 lakini hautoi huduma.

Vilevile, amesma DART wamekalia bidhaa za Sh. bilioni 3.43 za mifumo ya kukusanya nauli, CAG akionesha kuwa DART ilinunua kadi janja za Sh. bilioni moja na mifumo mingine ya TEHAMA ya kukusanyia nauli ya Sh. bilioni 2.43 vimetelekezwa.

"Pia kuna utoaji huduma usioridhisha. CAG ameonesha kati ya mabasi 210 ya mkataba, mabasi 132 (asilimia 63) yalikuwa mabovu na hayatoi huduma na kwamba yanahitaji Sh. bilioni 2.1 za matengenezo, lakini hazijatolewa. Yapo yanaoza, wanakimbilia kutoa zabuni kwa mwekezaji kutoka nje.

"Hoja zote alizotoa CAG ni hoja zinazotokana na uzembe wa kiutendaji na kimenejimenti na zina harufu ya uhujumu uchumi. Hii inasababisha kukosekana kwa thamani halisi ya fedha na kutotatua tatizo la usafiri jijini Dar es Salaam," amesema.

"ACT Wazalendo tunapendekeza Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI ajiuzulu kwa kushindwa kuisimamia DART na kusababisha hasara kubwa kwa Taifa. Pia Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI pamoja na bodi ya wakurugenzi wa DART na wahusika wengine wote wafikishwe mahakamani kwa makosa ya kuhujumu uchumi," amesema.

Waziri Mkuu Kivuli huyo alizungumzia Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP), akigusia kutotolewa fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR) Sh. bilioni 270 (asilimia tatu ya fedha za mradi).

Chama hicho pia kimeitaka serikali kulipa Sh. bilioni 208 za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambazo ilizichukua kama mkopo tangu mwaka 2020. Kimebainisha kuwa CAG pia ameonesha kuwa hadi kufikia 30 Juni 2023, NHIF imekusanya Sh. bilioni 5.6 (12.6%) pekee kati ya Sh. bilioni 42.57 inazozidai taasisi za serikali na binafsi ikiwa ni michango ya wanachama.

Kati yake, michango ambayo zinadaiwa taasisi za serikali ni Sh. bilioni 19.04 (45%) na Sh. bilioni 23.53 (55%) zinajumuisha madeni kutoka kwa mashirika yasiyo ya kiserikali.

Chama hicho pia kimeitaka serikali imilikishe Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ndege zote inazokodishiwa na kurejesha Wakala wa Ndege (TGFA) chini ya Wizara ya Uchukuzi kutoka Ofisi ya Rais.

Pia kimemtaka CAG kufanya ukaguzi maalum wa ununuzi wa ndege tangu ulipoanza mwaka 2016 hadi sasa.