Biteko apongeza mchango kanisa kwa maendeleo

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 01:00 PM May 05 2024
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.
PICHA: MAKTABA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amepongeza mchango wa kanisa katika maendeleo ya jamii na kuwashauri wachungaji kuwa na maono makubwa katika kuongoza waumini ili kujenga taifa la watu wenye mwelekeo chanya.

Biteko amesema hayo jijini Dodoma wakati wa kufunga kikao cha mazungativu (Retreat) kwa wachungaji wa Kanisa la FPCT.

Amesema ili waumini wapate uelekeo wa kwenda mahali fulani, wanahitaji mtu mmoja miongoni mwao atakayewaongoza kufikia malengo waliyojiwekea kutokana na maono aliyo nayo.

“Wachungaji msihangaike na wingi wa watu mahali popote. Angalia  uwezo wa kiongozi anayeona mbali atawaongoza wafike mbali.

“Askofu Mkuu umechagua fungu jema kufanya wachungaji hawa wakutane hapa  kujiongezea maarifa kwa kuwa tuko katika dunia iliyojaa utandawazi na  mafundisho ya  kweli na yasiyo ya kweli. Ni vigumu kwa waumini kutambua ya kweli na yasiyo ya kweli  hivyo,  wanahitaji kuongozwa,” amesema.

Aidha, Dk. Biteko amewahimiza viongozi wa dini kuwaongoza waumini kiroho na kuchagua viongozi sahihi wanaofahamu kuwa  watawaletea  maendeleo na ustawi wa nchi.
 
 Pia amewaomba viongozi wa dini kuwahimiza waumini kufanya kazi kwa bidii, kuhubiri kuhusu amani pamoja na kusisitiza maadili kwa waumini.

Dk. Biteko ametaja mafanikio mbalimbali ya serikali huku akiwaomba wachungaji hao kuendelea kumuombea na kumtia moyo ili aendelee kutekeleza miradi ya nchi katika maeneo mbalimbali.

“ Mradi wa reli ya kisasa (SGR) ni mkubwa. Haikuwa rahisi kupata fedha za kutekeleza mradi huu lakini Rais Samia Suluhu hassan amefanikiwa. Mradi wa ujenzi wa Bwawa la Julius  Nyerere unaozalisha megawati 2,115 umefanikiwa. Pia serikali imejenga madarasa, zahanati, vituo vya afya na kutoa ajira kwa watumishi wa sekta ya afya, angalieni nia yake, muungeni mkono,” amesema.

Pia amesema serikali inatambua umuhimu wa dini na imani za watu hivyo viongozi wa dini wahimize waumini kuchagua viongozi wanaofaa.

“Mwaka huu tuna uchaguzi wa serikali za mitaa. Viongozi  wa dini mna uwezo wa kuwahamasisha waumini waweze kuchagua viongozi wanaowahitaji kwa ajili ya kuwaletea maendeleo,” amesisitiza.