Bob Wangwe ajitosa msuguano CHADEMA

By Enock Charles , Nipashe Jumapili
Published at 11:23 AM May 05 2024
MKURUGENZI wa Jukwaa la Katiba  Tanzania (JUKATA) Bob Wangwe.
PICHA: MAKTABA
MKURUGENZI wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) Bob Wangwe.

MKURUGENZI wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) na kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bob Wangwe, ameshauri na kutoa mbinu katika kumaliza msuguano unaodaiwa kuwamo ndani ya chama hicho.

Amependekeza kuwapo makubaliano baina ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, na Makamu Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, kuhusu nani anafaa zaidi kugombea nafasi ya urais mwaka 2025 ili kuepusha misuguano baina ya wanachama.

Katika taarifa yake iliyosambaa katika mitandao ya kijamii, Wangwe ambaye ni mwanasheria kitaaluma, amedai kuwa, kwa ushahidi wa kimazingira unaonyesha viongozi hao wawili wamedhamiria kugombea urais mwakani.

Amesema kutokana na hilo, anawashauri wanachama wa chama hicho kutokuwa na upande baina ya viongozi hao, bali kusimama na chama ili kuepusha mivutano.

“Kwa uthibitisho wa kimazingira Freeman Mbowe na Tundu Lissu, wote wamenuia kugombea urais ifikapo 2025, viongozi hawa wawili wana ushawishi na wote wanaweza kugombea na kushinda au kuleta ushindani mkubwa.

“Tukikubali kuchukua upande baina ya viongozi hawa, itamaanisha kuchukua upande wa migawanyiko na kuchafua viongozi wetu, imani yangu ni kwamba, mgombea urais CHADEMA ataamuliwa na Tundu Lissu na Freeman Mbowe wenyewe kabla ya taratibu zingine za chama kuendelea,” amesema Wangwe katika taarifa hiyo.

Kada huyo amedai chama hicho kikuu cha upinzani nchini kwa sasa kimekuwa na wanachama wengi kiasi cha watu mbalimbali kutamani kuwania nafasi za uongozi ndani ya chama na zile za kiserikali.

Amesema hatua hiyo imeondokana na utaratibu uliokuwapo miaka ya nyuma wa watu kubembelezwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Kwa mara ya kwanza chama hicho kusimamisha mgombea wa urais tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa ilikuwa ni mwaka 2005 ambao Dk. Jakaya Kikwete (CCM) alishinda na Prof. Ibrahimu Lipumba  kushika nafasi ya pili, huku Mbowe akiwa wa nafasi ya tatu kwa matokeo.

Mwaka 2010, CHADEMA kilimsimamisha Dk. Wilbroad Slaa, aliyepata kura zaidi ya milioni mbili sawa na asilimia 26 akishika nafasi ya pili nyuma ya Dk. Kikwete aliyepata kura zaidi ya milioni tano, sawa na asilimia 61, katika uchaguzi uliokuwa na mchuano mkali baina ya CCM na CHADEMA.

Mwaka 2015, chama hicho kilimsimamisha Hayati Edward Lowassa kuwa mgombea urais kupitia UKAWA ukijumuisha vyama vya CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, na kushika nafasi ya pili nyuma ya Hayati Dk. John Magufuli, aliyetangazwa mshindi.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 katika nafasi ya urais, chama hicho kilimsimamisha Makamu Mwenyekiti  wa chama hicho, Tundu Lissu, aliyechuana vikali na Hayati Magufuli na kushika nafasi ya pili katika uchaguzi uliolalamikiwa na wadau mbalimbali  kuwa haukuwa huru na wa haki.