CBE yaja na program ya uanagenzi

By Frank Monyo , Nipashe Jumapili
Published at 08:14 AM Apr 21 2024
Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Tandi Lwoga (kulia) akimkabidhi tuzo mgeni Rasm, Edward Talawa ambaye ni Mkurugenzi mkuu wa FINCA Microfinance Bank kwa kushiriki siku ya Atamizi (Incubation) mwishoni mwa wiki na kufungua milango kwa CBE.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Tandi Lwoga (kulia) akimkabidhi tuzo mgeni Rasm, Edward Talawa ambaye ni Mkurugenzi mkuu wa FINCA Microfinance Bank kwa kushiriki siku ya Atamizi (Incubation) mwishoni mwa wiki na kufungua milango kwa CBE.

CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kinakusudia kuanzisha mafunzo ya uanagenzi kwa wanafunzi wanaosoma shahada ya masuala ya benki na fedha, metrolojia na viwango, ambayo yatawawezesha kusoma huku wakifanyakazi.

Akizungumza katika siku ya CBE taaluma na rogramu atamizi jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edda Lwoga, alisema lengo ni kuwawezesha wanafunzi kuhitimu masomo wakiwa na ujuzi unaohitajika kwenye soko la ushindani wa ajira.

Alisema katika utaratibu huo, mwanafunzi atasoma muhula mmoja chuoni na muhula mwingine kwa mwajiri, ambako utakuwa anapata mafunzo kwa vitendo.

“Kwa hiyo mwanafunzi atasoma mwaka mmoja na nusu chuoni na mwaka mmoja na nusu kwa mwajiri. Tumeshaingia makubaliano na baadhi ya taasisi ambazo ziko tayari kuwapokea wanafunzi kwa mafunzo ya vitendo,” alisema.

Kuhusu uatamizi, Profesa Lwoga alisema lengo la programu hiyo ni kuwawezesha wanafunzi kuwa wabunifu na kutumia elimu ya darasani kutengeneza biashara halisi.

Alisema wanapatiwa mafunzo sahihi kuhusu mawazo yao ya biashara, mitaji na kuwaunganisha na wafanyabiashara pamoja na taasisi zinazohusika na ubunifu wao.

Alisema tayari wanafunzi 282 wameshaanza program atamizi   na  wameanza kutengeneza bidhaa na mifumo ya kutatua changamoto mbalimbali kwa jamii.

Akizungumza katika tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Finca, Edward Talawa, ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema moja ya nyenzo muhimu ambayo wabunifu wanapaswa kuwa nayo ni nidhamu ya fedha na kwamba benki yake itatoa nafasi ya uanagenzi kwa wanafunzi wa CBE.

Alisema ubunifu uliofanywa na CBE utasadia kutatua changamoto ya ajira nchini, kwa kuwa itazalisha wajasiriamali ambao watajiajiri na kuajiri wengine.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Ushirika wa wajasiriamali wahitimu wa Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA), Revocatus Kimario, alisema wanafunzi wana nafasi ya kupata masomo ya vitendo katika nchi za Ulaya na kuwataka walio katika programu ya uatamizi kuzichangamkia.

Kwenye siku hiyo ya taaluma na program atamizi, wanafunzi wa chuo hicho walionyesha uwezo mkubwa kwenye ubunifu wa teknolojia mbalimbali.

Wanafunzi hao walionyesha ubunifu kwenye utengenezaji wa bidhaa mbalimbali na mifumo mbalimbali ya kiteknolojia inayoweza kutumika kutatua changamoto mbalimbali kwenye jamii.