Mbaroni madai kulaghai watu kazi

By Romana Mallya , Nipashe Jumapili
Published at 12:24 PM May 05 2024
Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna Msaidizi mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro.
PICHA: MAKTABA
Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna Msaidizi mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro.

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watuhumiwa 10 akiwamo raia wa Kenya kwa tuhuma mbalimbali zikiwamo kujifanya wakala wa mafunzo ya biashara na kujipatia fedha na anayetumia picha za viongozi kuwalaghai watanzania atawapatia kazi na uhamisho.

Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna Msaidizi mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro, ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu operesheni maalum iliyoanza mwezi uliopita.

Amesema katika operesheni hiyo, walimkamata, Hassan Chambilia Sumilanda (28)  maarufu Dk. Hassan Mangena, mkazi  Sinza Kumekucha, anayetumia picha za viongozi wakuu serikalini kuwalaghai watanzania kuwa atawasaidia kupata kazi na uhamisho.

Amesema mtuhumiwa huyo anatuhumiwa kufanya hivyo ili kujipatia fedha kwa njia ya udangayifu kwa kudai kuwasaidia watu kupata kazi au uhamisho jambo ambalo siyo la kweli. 

“Mtuhumiwa huyu amekuwa akitumia fursa mbalimbali za hafla za kiserikali kupiga picha na viongozi wakubwa wa serikalini na kuziweka katika kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii kwa jina la Hassani Mangena na kujitambulisha kuwa ni mtumishi wa serikali kutoka Wizara ya Afya, Kitengo cha Mama na Mtoto.

“Wakati mwingine hujitambulisha kuwa ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu,” amesema. 

Kamanda Muliro amesema wanawahoji watuhumiwa wengine wanne ambao ni Javani Ochengi (36), raia wa Kenya, anayeishi Kimara, Yohana Mroso (20), mkazi wa Mbagala, Fransis Asangwile (34), mkazi wa Kongowe na Auston Mpanju (32), mkazi wa Tuangoma,  wanatuhumiwa kujipatia fedha kwa udanganyifu.

Amesema watuhumiwa hao wamekuwa wakijinadi kuwa wao ni wakala wa mafunzo ya biashara na kwamba, watawatafutia vijana shule, vyuo, kazi au sehemu za utalii nje ya nchi.

“Watuhumiwa hao wamekuwa wakitumia kampuni ijulikanayo kwa jina la PROFFESION EXCHANGE PLATFORM (PEXPLA) kuwahadaa watu walipe fedha ili wasaidie kupata nafasi wanazohitaji, kitendo kilichowezesha kukusanya kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwa wananchi kisha kutoweka,” amesema.

Kamanda Muliro pia, amesema wanamshukilia, Essau Fransis (27), maarufu Makumba mkazi wa Makumbusho na wenzake wanne wakiwa na luninga 35 zilizoibwa katika maeneo mbalimbali Dar es Salaam na sita kati yake zimeshatambuliwa. 

Amesema Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa  za kweli na linaahidi kuzitunza kwa siri na halitakuwa na huruma kwa mtuhumiwa yeyote anayejihusisha na vitendo vya kihalifu.