Mwananchi amzawadia 5,000/- Rais Samia

By Munir Shemweta , Nipashe Jumapili
Published at 12:43 PM May 05 2024
Noti ya shilingi 5,000.
PICHA: MAKTABA
Noti ya shilingi 5,000.

MKAZI wa kijiji cha Luchima katika kata ya Majimoto, Halmashauri ya Mpimbwe, Mlele mkoani Katavi, Aseni Jandikile, amemzawadia Sh. 5,000 Rais Samia Suluhu Hassan kwa kile alichosema ni kutokana na juhudi zake za kuwaletea maendeleo wananchi.

Kiasi hicho cha pesa alikikabidhi kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda, ambaye ni Mbunge wa Kavuu, wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Luchima wakati wa ziara yake ya kuwafariji wananchi waliopatwa na mafuriko katika jimbo hilo.

‘’Nampongeza Rais kwa vitendo kabisa. Naomba Mheshimiwa Mbunge nikukabidhi fedha taslimu Sh. elfu tano umpelekee Mheshimiwa Rais, ’’ amesema.

Kwa mujibu wa mwananchi huyo, uamuzi wake unatokana na kuvutiwa na uongozi bora na utendaji kazi wa Rais Samia hasa kwa kuwajali wananchi wa Luchima. Alisema pamoja na mambo mengine, amewajali kwa kutoa Sh. milioni 50  kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ambayo alisema imewakomboa wananchi wa kijiji hicho.

Naibu Waziri Pinda amesema fedha hizo zilizotolewa na mwananchi huyo, zitamfikia Rais Samia. 

Pinda amempongeza mwananchi huyo kwa uamuzi wake wa kutoa kiasi hicho cha fedha kama ishara ya kukubali juhudi na kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Luchima na Tanzania kwa ujumla.

Amewaeleza wananchi wa kijiji hicho kuwa Rais Samia anawapenda na amekuwa akisaidia juhudi mbalimbali za maendeleo kwenye jimbo la Kavuu na kutaja baadhi ya juhudi hizo kuwa ni pamoja na kutoa fedha za ujenzi wa hospitali, shule, barabara pamoja na upatikanaji wa huduma za maji.

Pinda amefanya ziara katika jimbo la Kavuu kuwafariji wananchi waliopatwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyoathiri pia miundiombinu yakiwamo madaraja.