Safari za majini zarejea baada ya kimbunga ‘Hidaya’ kutoweka

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 01:51 PM May 05 2024
Safari za majini zarejea.
PICHA: MAKTABA
Safari za majini zarejea.

BAADA ya kujiridhisha kuwa hali ya hewa imetulia na upepo kupungua, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeruhusu usafiri wa majini kuendelea kama kawaida.

Usafiri wa meli na boti kutoka Unguja kwenda Dar es Salaam, Unguja kwenda Pemba na Pemba kwenda Tanga ulizuiwa tangu jana Mei 4, 2024 saa moja asubuhi kutokana na upepo mkali ulioanza kuvuma saa 3.00 usiku wa Mei 3, 2024 uliosababishwa na kimbunga Hidaya.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kimbunga hicho kilipoteza nguvu kadri kilivyokuwa kikisogea nchi kavu.

Akizungumza na chombo kimoja cha habari leo Mei 5, 2004 Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), Sheikha Ahmed Moh'd amesema baada ya kujiridhisha na utulivu wa hali ya hewa wameruhusu safari ziendelee.

Kwa upande wa Dar es Salaam, leo Jumapili Mei 5, 2024 katika maeneo ya Posta, shughuli za usafiri wa boti kuelekea Unguja ziliendelea kama kawaida kuanzia saa moja asubuhi.

Msimamizi wa Uendeshaji Boti za Kilimanjaro, Ally Juma amesema wamerejesha usafiri baada ya mamlaka husika kuwaruhusu kutokana na hali ya hewa kutengamaa tofauti na jana Jumamosi Mei 4, 2024.