Takwimu mguu kifundo, mgongo kupinda zashtua

By Romana Mallya , Nipashe Jumapili
Published at 12:12 PM May 05 2024
Meneja wa Kitengo cha Upasuaji Mifupa na Viungo Watoto MOI, Dk. Bryson Mcharo.
PICHA: MAKTABA
Meneja wa Kitengo cha Upasuaji Mifupa na Viungo Watoto MOI, Dk. Bryson Mcharo.

TAKWIMU za watoto wanaozaliwa na mguu kifundo, mgongo kupinda na mtindio wa ubongo ambao wengi hupokewa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wakiwa wamecheleweshwa, imeshtua na kuanza kuwasaka mitaani.

Kwa mujibu wa wataalam, ucheleweshaji huo husababisha mtoto kufanyiwa upasuaji ambao hubaki na maumivu maisha yake yote, wakati angewahishwa angepona.

Meneja wa Kitengo cha Upasuaji Mifupa na Viungo Watoto MOI, Dk. Bryson Mcharo, ambaye ni Bingwa Mbobezi Upasuaji Mifupa na Viungo Watoto, ameyasema hayo kupitia mahojiano maalum na mwandishi wa habari hizi.

Dk. Mcharo amesema kutokana na ongezeko hilo,  MOI imeanza kuwasaka mtaani kupitia programu maalum iliyoanza Mei Mosi, mwaka huu, kwa kuendesha huduma ya tiba ya mifupa na viungo kwa watoto mikoa mbalimbali.

Amesema wameamua kufanya hivyo kwa kuwa, kati ya watoto wanaofikishwa hospitalini hapo, baadhi huangukia kwenye upasuaji kutokana na kucheleweshwa.

Amesema taasisi hiyo ina kliniki tatu kwa wiki zinazofanyika siku za Jumatatu, Jumatano na Alhamis ambapo Jumatano imetengwa kwa ajili ya miguu kifundo na hupokea watoto kati ya 10 hadi 30.

“Siku ya Jumatatu tunapokea kati ya 80 hadi 100 na wengi wao ni wale wanaendelea na kliniki, wapya huwa kati ya 10 hadi 15. Mtoto anapowahishwa hospitalini mapema anaweza kuchukua takribani wiki nne hadi sita hadi kufikia kuvalishwa kiatu. Na kuwahi inasaidia mguu kutibika.

“Changamoto huja mtoto anapocheleweshwa hospitalini itabidi upasuaji na atakuwa na kovu, kunyoosha mifupa ambapo hatua hizi zinaweza kukuletea maumivu baadaye. Unaweza ukatibu ulemavu, lakini ukabaki na tatizo la maumivu maisha yote,” amesema.

Dk. Mcharo amesema changamoto nyingine ambayo atakutana nayo ni unyanyapaa mpaka miaka 10 hadi 20 na kuleta shida ya kisaikolojia kwa mhusika.

Amebainisha kuwa, watoto wanaowapokea kwenye kliniki hospitalini hapo ni mpaka umri wa miaka 16, kwa kuwa wasichana wanakoma kukua mifupa yao mpaka miaka 14 na wavulana mpaka miaka 16 wanaendelea kukua.

Dk. Mcharo amesema waliandaa programu ya kuwafikia watoto hospitalini hapo siku ya Mei Mosi iliyokutanisha watoto na madaktari bingwa wa mifupa, ambayo lengo lake lilikuwa ni kuwaona watoto kati ya 100 hadi 200, lakini waliofika wagonjwa wapya watoto 126.

Amesema waliamua kuendesha programu hiyo kwa kuwa, MOI imekuwa ikiendelea kuwapokea watoto hao wakiwa wamecheleshwa matibabu.

“Wangekuja mapema, wangepata matibabu kwa gharama rahisi kwao, kwa taasisi na serikali kwa ujumla, lakini kwa sababu zilizo nje ambazo hatujazijua, kumekuwa na ucheleweshaji wa watoto kufika hospitalini.

“Wengi wanakuja wamechelewa, ama wamepata matibabu ambayo si sahihi huko. Kama idara tumeona tutoe elimu na kufanya kliniki ambapo pamoja na kuwasaidia, huduma itawafikia watanzania wengi ili wawalete watoto hospitalini mapema,” amesema.

Dk. Mcharo amesema wengi wao waliowahudumia siku ya Mei Mosi, ni wale waliokuwa nyumbani ambao hawajawahi kutibiwa matatizo yao.

Amesema miongoni mwao wapo wenye matatizo ya mguu kifundo, wenye utindio wa ubongo unaopelekea kupata matatizo ya nyonga, mifupa ambao walikuwa wengi.

“Tunapoongelea matatizo ya mifupa kwa watoto wadogo, huanzia pale mtoto anapozaliwa, kuna uwezekano wa watoto kuzaliwa nayo, mfano mguu kifundo, takwimu zinaonyesha katika watoto wanaozaliwa 750 mpaka 1,000.

“Tukichukuliwa idadi ya watu kwa Tanzania, tunaweza kuona kwa namna gani kuna watoto wangapi waliozaliwa na matatizo haya takwimu zinaonyesha ni asilimia moja mpaka tano ya watanzania wote.

“Kwa hiyo tuna zaidi ya watu 600 wako mahali na inawezekana hawajatibiwa kabisa kwa kuwa, tunapata watoto ambao hawajawahi kutibiwa na migongo imepinda upande,” amesema.

NINI CHANZO?

Dk. Mcharo amesema yako matatizo ambayo mtoto hupata wakati wa ukuaji wake, kama upungufu wa lishe au Vitamin D inayosababisha kupata matege.

Pia ametaja kundi lingine la ukuaji wa mtoto ambao haushabiani  kati ya upande wa ndani wa mfupa na nje na kusababisha kupinda miguu.

Amesema watoto wa aina hiyo ni wengi kwa kuwa, wakiangalia takwimu zilizowahi kutolewa duniani, wanaona kuna watoto wengi wanazaliwa na matatizo hayo.

“WaKo wanaopata wakati wa ukuaji, tunapoongelea maambukizi katika mfupa , maungio  hawa watoto wapo wengi sana.

“Tumeona si busara kukaa na kupokea watoto ambao wanafikishwa hapa wakiwa wamecheleweshwa. Tukiangalia mifumo ya nchi nyingine wamekuwa wakiendesha hizi programu kwa kutoka nje ya taasisi na kuwapata watoto mapema na wananchi nao wanapata elimu ya kuwawahisha hospitalini mapema,” amesema.

Mtaalam huyo amesema wameanza programu hiyo Mei Mosi na kwa Mkoa wa Dar es Salaam, wataendelea Mbagala, Gongo la Mboto, Tegeta na baada ya hapo watazunguka nchi nzima ikiwamo mikoa ya Morogoro na Tanga.

Amesema waKo watoto ambao hupokewa MOI kupitia taasisi zisizo za kiserikali ambao wengi wao huwa hupatikana mitaani wakiwa wamezidiwa na hawajiwezi.

“Hata jamii inawaona, lakini inashindwa kujua iwapelekea wapi, tunafikiri kupitia programu hii tutafikia watanzania wengi. Tunaomba watanzania watuunge mkono ili kuzuia ulemavu wa aina hii unaotibika,” amesema.