Wahitimu watakiwa kuzingatia masomo ili kupata ufaulu mzuri

By Gideon Mwakanosya , Nipashe Jumapili
Published at 05:24 PM Apr 21 2024
Pichani kulia ni Brigedia Jenerali Charles Feruzi Mkuu wa Jeshi la Wananchi Wa Tanzania JWTZ Brigedi ya Kanda ya Kusini akiwa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Ruhuwiko LT COL Benedicto Bahame pichani kushoto wakati wa Mahafali ya 19 ya Kidato cha sita.
Picha: Gideon Mwakanosya.
Pichani kulia ni Brigedia Jenerali Charles Feruzi Mkuu wa Jeshi la Wananchi Wa Tanzania JWTZ Brigedi ya Kanda ya Kusini akiwa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Ruhuwiko LT COL Benedicto Bahame pichani kushoto wakati wa Mahafali ya 19 ya Kidato cha sita.

BRIGEDIA Jenerali Charles Peter Feruzi wa Jeshi La Wnanchi wa Tanzania (JWTZ) Kanda ya kusini amewataka wahitimu wa kidato cha sita wa shule ya Sekondari ya Ruhuwiko Manispaa ya Songea inayomilikiwa na Jeshi hilo kuona umuhimu wa kuzingatia zaidi masomo waliyoyapata kwa kipindi chote ambayo yataweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa kufanya mitihani inayo tarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Ushauri huo umetolewa na Brigedia Jenerali Charles Peter Feruzi kwenye mahafali ya 19 ya kidato cha sita yaliyofanyika kwenye ukumbi mpya wa mikutano wa shule hiyo yaliyohudhuriwa pia na wazazi wa wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya kidato cha sita hivi karibuni.

Amesema kuwa ni wajibu wa kila mwanafunzi kuona namna ya kujitahidi kufanya vizuri zaidi katika mitihani ya kidato cha sita inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni na hasa ikizingatiwa kuwa shule ya sekondari Ruhuwiko kwa muda mrefu imekuwa ikifanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kidato cha sita na si vinginevyo.

Ameongeza kuwa kitaaluma shule ya Sekondari Ruhuwiko iko vizuri hivyo anaamini kuwa baada ya kufanya mitihani hiyo matokeo yatakuwa mazuri na kuendelea kuleta sifa nzuri ya shule hiyo na ameupongeza uongozi wa shule ya sekondari hiyo pamoja na Walimu kwa kuhakikisha kuwa taaluma kwa wanafunzi wao inaleta matuaini mazuri kwa jamii.

Mkuu wa Shule Ruhuwiko LT COL Benedicto Bahame mapema akitoa taarifa ya utendaji wa shule hiyo kwa mgeni rasmi katika mahafali ya kidato cha 6 Brigedia Jenerali Charles Peter Feruzi amesema kuwa shule ya Sekondari ya Ruhuwiko ni miongoni mwa shule 10 zinazomilikiwa na Jeshi la ulinzi wa Tanzania hapa nchini ambazo alitaja shule hizo kuwa ni Airwing,Ali Khamis Camp, Jitegemee, Kawawa, kigamboni, Kizuka, Makongo, Nyuki, Ruhuwiko na Unyenyembe na kwamba shule hiyo ni ya mchanganyiko kwa wavulana na wasichana ikiwa ni ya bweni na kutwa kuanzia shule ya awali,Msingi,kidato cha 1 hadi cha 6.

Amesema kuwa shule ya sekondari ya Ruhuwiko ilianzishwa mwaka 1979 awali ikijulikana kwa jina la Huduma JWTZ Center na kimsingi ilianza ikiwa na kituo cha kufanyia mitihani na ilianzishwa kwa lengo la kuwaendeleza askari wa Jeshi la wananchi ambao hawakuwa wamefikia elimu ya kidato cha nne kwa wakati huo baada ya lengo la JWTZ la kusomesha askari wake angalao kufikia kidato cha 4 kufanikiwa kwa asilimia kubwa na kufutwa rasmi kwa mpango huo uongozi wa Jeshi la Wananchi Tanzania JWTZ uliona ni busara kundelea kutoa huduma za shule kwa familia za Jeshi na raia.

LT COL Bahame amesema kuwa maendeleo ya taaluma katika shule yake yamekuwa yakiimarika mwaka hadi mwaka ambapo shule hiyo imekuwa na maendeleo ya kitaaluma na hasa kwa upande upande wa kidato cha 5 na 6 kwani shule hiyo imepata tuzo zawadi na zawadi kwa nyakati tofauti ambapo alitoa mfano kuwa mwaka 2020 shule hiyo ilitunukiwa tuzo na cheti na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo kwa wakati huo kwa kuwa shule ya 9 kitaifa miongoni mwa shule zilizoboresha ufaulu kwa kiwango cha juu kwenye mitihani ya kidato cha 6 mwaka 2020.

Amesema kuwa mwaka 2021 hadi 2023 matokeo ya kidato cha 6 yameendelea kuwa mazuri zaidi na kufanya shule hiyo kuwa ya kwanza mfululizo kati ya shule 8 za kadato cha 5 na 6 zinazomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania ambapo matokeo hayo ya kidato cha 6 yameendelea kuwa mazuri zaidi kwa miaka mingi mfululizo na mwaka 2023 shule hiyo imefanikiwa kabisa kufuta daraja la 3 kwa kupata ufaulu wa daraja la 1 na la 2 na lengo la shule hiyo kwa sasa ni kuwa na ufaulu wa daraja la kwanza tu na si vinginevyo.