Lowassa ameacha funzo kubwa kwa Watanzania, wajifunze sasa

Nipashe Jumapili
Published at 05:31 PM Feb 18 2024

HATIMAYE Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, amemaliza safari ya maisha yake duniani, baada ya jana kuzikwa nyumbani kwake, Monduli mkoani Arusha. Lowassa alifariki dunia Jumamosi iliyopita katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu.


Tangu kutokea kwa kifo chake, watu mbalimbali walizungumza mambo mazuri aliyoyafanya kwa taifa katika nafasi mbalimbali alizoshika katika serikali na utumishi wa umma, zikiwamo Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Miji, Waziri wa Maji na Mifugo, na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais. 

Wanasiasa wakongwe na walioko madarakani pamoja na viongozi wa dini, walitoa kauli mbalimbali zinazomwelezea kuwa alikuwa mtu wa watu kutokana na kujali kwake watu wanyonge na kuwasaidia. Hakuwa mbaguzi wa imani kwa kuwa hata alipoalikwa kwenye hafla mbalimbali za kuchangia maendeleo ya taasisi za dini, alikubali na kutoa michango yake kwa uzito ule ule. 

Ni kweli kwamba katika nafasi za uongozi alizoshika, Lowassa alionyesha uwezo wake wa hali ya juu ikiwa ni pamoja na kupanga, kusimamia kile alichokiamini kwamba kina manufaa na matokeo chanya yanayotarajiwa. Katika kuhakikisha anayoyapanga yanatekelezwa, kwa watendaji alikuwa akitumia maneno nataka, naagiza na tekeleza. Neno kwamba naomba kwake ulikuwa msamiati mgumu.

Katika sekta zote alizosimamia, matokeo yalionekana na alipokuwa Waziri Mkuu, kutokana na nafasi hiyo kuwa ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za serikali, alizunguka kila sekta na kuhakikisha yale wanayokubaliana yanatekelezwa. Wale walioshindwa kuyatekeleza hakuwa na mswalie mtume nao, aliwaondoa bila kujali ni watu wa namna gani. 

Watu walishuhudia jitihada zake katika maendeleo ya elimu ya sekondari baada ya kuanzishwa kwa shule za kata hasa baada ya wanafunzi kuongezeka huku miundombinu ikiwa haijakamilika. Alikutana na wakuu wa mikoa na kuagiza kuwa ndani ya muda mfupi waliojiwekea kazi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa iwe imekamilika. Hakuagiza tu bali aliwaambia ukweli kwamba atakayeshindwa kufanikisha hilo afungashe.

Kwa jumla Lowassa alikuwa mtu wa kuthubutu kutokana na kiu yake ya kutaka mambo yafanikiwe. Hata taifa lilipoingia katika mgawo wa umeme, alitafuta suluhu ya kutafuta kampuni za kufua umeme ili nchi isiwe gizani. Yaliyotokea kuhusu Richmond ni historia lakini alionyesha moyo wa kuthubutu ili kuhakikisha nchi inapata nishati hiyo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Lowassa pia alikuwa mvumilivu na mtu wa kupenda amani. Hilo lilijidhihirisha mwaka 2015 baada ya matokeo ya urais yaliyompa John Magufuli (naye sasa marehemu) ushindi wa urais. Kulikuwa na madai kwamba Lowassa alikuwa ameshinda uchaguzi huo na wafuasi wake walitaka kupinga lakini aliwaambia wamwachie Mungu. 

Alama nyingine kubwa ambayo Lowassa ameiacha ni maendeleo katika jimbo la Monduli aliloliongoza kwa takriban miaka 20. Kama zilivyo sehemu nyingi kame kwenye ukanda wa Umasaini, Monduli nayo ni mojawapo lakini alipambana kuhakikisha wananchi wanapata maji. 

Pia alipambana kuhakikisha Watoto wa jamii ya wafugaji wa kabila la Wamasai wanapata elimu na shule nyingi zilijengwa, si Monduli tu bali maeneo mengi ndiyo maana watu wa jamii hiyo walimlilia baada ya kusikia amefariki dunia. 

Kutokana na sifa hizo, Lowassa ameacha fumbo kubwa na elimu kwa viongozi kuwa wanapaswa kutanguliza maslahi ya umma na si binafsi. Hiyo ni tofauti na viongozi wengi ambao wamekuwa wakiingia katika nafasi za kisiasa kama ubunge na udiwani kwa kuwa baadhi wamekaa kwa muda mrefu lakini hakuna maendeleo kwenye maeneo hayo na watu wao wanaishi katika umaskini uliotopea. 

Ni wazi kwamba  kama kila kiongozi anayepewa dhamana ama kwa kuchaguliwa au kuteuliwa katika nafasi fulani atatekeleza wajibu wake ipasavyo, hakika Tanzania itaupiga teke umaskini. Lowassa ameacha funzo kubwa kwa viongozi na Watanzania kwa ujumla. Tujifunze kutoka kwake.