Uamuzi wa kufuta leseni madini mwafaka, sheria iogezewe makali

Nipashe Jumapili
Published at 02:53 PM Mar 24 2024
Waziri wa Madini, Athony Mavunde.
PICHA: WIZARA YA MADINI
Waziri wa Madini, Athony Mavunde.

MADINI ni moja ya sekta muhimu kwa maendeleo endelevu ya nchi pamoja na pato la taifa. Hiyo ni kutokana na Tanzania kujaliwa kuwa na aina mbalimbali za madini na vito ambavyo kama vitasimamiwa ipasavyo, vinaweza kuupaisha Uchumi wa nchi kwa kiwango kikubwa.

Mchango wa sekta hiyo kwa maendeleo ya Uchumi umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka, hivyo kuonyesha kuwa ni moja ya maeneo ambayo ni tegemeo katika kuifanya Tanzania kuendelea kupaa kimaendeleo na hata kuchangia ongezeko la fedha za kigeni kwa kuuza nje ya nchi. 

Takwimu zinaonyesha kwamba mchango wa sekta hiyo kwa mwaka 2021 ulikuwa asilimia 7.2 ikilinganishwa na asilimia 4.4 ilivyokuwa mwaka 2017 likiwa ni ongezeko la asilimia 2.8. Pia katika robo ya tatu ya mwaka 2022/23 mchango wa sekta ya madini ulifikia asilimia 9.6. 

Aidha, serikali katika kipindi hicho, kupitia sekta ya madini, ilikusanya Sh. bilioni 409.66 sawa na asilimia 85.43 ya lengo la mwaka la kukusanya Sh. bilioni 479.51 katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2022/2023. Hayo ni matokeo makubwa ambayo yanaonyesha kuwa sekta hiyo ni muhimu katika uchumi wa nchi.  

Kutokana na maono ya serikali ya awamu ya tano katika sekta hiyo, mkazo mkubwa uliwekwa kwa kuwapo kwa masoko ya madini nchini pamoja na kuwapo kwa mitambo ya uchakataji ili kuyapa thamani badala ya kupeleka yakiwa ghafi kupitia makinikia ambayo yalikuwa hayabainishi kiasi halisi cha madini yaliyomo. 

Aidha, kwa kutambua umuhimu wa madini, serikali iliweka jitihada za usimamizi madhubuti kuanzia utafiti, uchimbaji hadi mauzo kwa kuanzishwa kwa Tume ya Madini. Matokeo ya kuundwa kwa tume hiyo pamoja na wizara inayosimamia sekta hiyo yalianza kuonekana kwa kuongezeka mapato ya ukuaji wa sekta kwa ujumla. 

Pamoja na jitihada hizo za serikali, imebainika kuwa wako baadhi ya watu sita wenye leseni za utafutaji wa madini, wakiwamo wanaomiliki ekari milioni 13.5 lakini hawazifanyii kazi. Pia imebainika kuwa katika leseni hizo kuna mtu mmoja ambaye pekee yake ana maombi 973 ya leseni  ambazo zina eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 23,118 lakini hafanyi kazi bali amezishikilia tu.

Hatua hiyo imesababisha serikali, kupitia Waziri wa Madini, Athony Mavunde kuagiza Tume ya Madini kufuta leseni 2,648 za watu mbalimbali, wakiwamo waliojitwalia maeneo makubwa bila kuyafanyia kazi.

Waziri Mavunde, akitoa agizo hilo, alisema kumekuwa na baadhi ya wamiliki wa leseni ambao wamekuwa hawazingatii utekelezaji wa majukumu yao ya umiliki kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura 123. Pia aliwaonya wanaoomba leseni kwa njia ya mtandao na kushindwa kuendeleza maeneo wanayopewa kuwa watachukuliwa hatua vinginevyo waache mara moja. 

Kitendo hicho cha wamiliki wa leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini kushindwa kuzitumia, inarudisha nyuma nia njema ya serikali katika kutumia rasilimali za nchi kwa maendeleo ya wananchi katika sekta mbalimbali. 

Ni wazi kwamba mapato yatokanayo na sekta hiyo, ni sehemu ya fedha zinazotumika katika maendeleo ya sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, maji na miundombinu, hivyo kitendo cha watu kuhodhi maeneo bila kuendeleza shughuli za uchimbaji hakikubaliki. Uamuzi uliochukuliwa na serikali wa kufuta leseni hizo ni mwafaka kwa sababu una lengo la kuleta maendeleo na watu hao wanaokwamisha maendeleo kwa kuhodhi leseni na kukalia maeneo, hawana tofauti na wahujumu uchumi.

Licha ya uamuzi wa serikali kufuta leseni hizo, liko jambo la kujifunza na linapaswa kuwekwa katika Sheria ya Madini kwa kutoa muda maalumu kwa mwombaji kuanza kufanya kazi baada ya kupatiwa leseni. Kinyume cha hapo, mtu huyo anyang’anywe leseni ili wapewe wengine wenye nia na uwezo wa kutafuta na hatimaye kuchimba madini ili kuiletea nchi maendeleo.