Bingwa kuogelea kupatikana leo

By Shufaa Lyimo , Nipashe Jumapili
Published at 11:48 AM Apr 21 2024
Mashindano ya kuogelea.
PICHA: MAKTABA
Mashindano ya kuogelea.

ZAIDI ya waogeleaji 100 kutoka mikoa mbalimbali nchini wanatarajiwa kushiriki mashindano ya Klabu Bingwa ya mchezo huo yatakayomalizika leo kwenye bwawa la kuogelea la Shule ya Kimataifa Tanganyika (IST) jijini, Dar es Salaam.

Akizungumza na Nipashe, Mratibu wa Habari wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Sebastian Kolowa, amesema mashindano hayo yatashirikisha klabu 11 kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar na nyingine moja kutoka Nairobi,  Kenya.

Kolowa amesema mashindano hayo yamepata baraka za Chama cha Dunia cha Kuogelea na waogeleaji watakaofanya vizuri watapata tiketi ya kushiriki michuano ya dunia itakayofanyika baadaye mwaka huu huko  Burgaria.

"Ushindani utachagizwa kutokana na kuwapo na waogeleaji wa kimataifa, Sophia Latif na Hilal Hilal, tunatarajia mashindano yatakuwa na upinzani mkubwa, tunakaribisha wadau mbalimbali wajitokeze," amesema Kolowa.

Kiongozi huyo amesema kila klabu iliyothibitisha kushiriki mashindano hayo ya mwaka huu imejipanga kufanya vizuri kutokana na maandalizi ya muda mrefu waliyofanya.