Rais Samia atunukiwa shahada ya Udaktari wa Heshima

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:14 PM Apr 18 2024
Profesa Necdet Unuvar akimkabidhi Shahada ya Udaktari wa Heshima Rais Samia Suluhu Hassan (kulia).
Picha: Ikulu
Profesa Necdet Unuvar akimkabidhi Shahada ya Udaktari wa Heshima Rais Samia Suluhu Hassan (kulia).

Chuo Kikuu cha Ankara kilichopo nchini Uturuki, kimekamilisha zoezi la kumtunuku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, Shahada ya Heshima (Honoris Causa) katika Uchumi, ikiwa ni ishara nzuri za kutambua juhudi zake za kuendeleza mageuzi ya kijamii, kisiasa na kiuchumi na kuiishi falsafa yake ya 4R.

Zoezi la kumtunuku Rais Samia limeendeshwa na Profesa Necdet Unuvar wa chuo hicho, ambapo pamoja na kutambua mchango wa Rais Samia, pia wameiheshimisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Samia amekishukuru Chuo Kikuu cha Ankara kwa kumpa heshima hiyo kubwa duniani, akisema ameipokea kwa furaha, akiamini uamuzi wao huo ni ishara njema kwa Taifa la Tanzania.

“Natoa shukrani zangu kwa Seneti ya Chuo Kikuu cha Ankara kwa uamuzi wa kunipa Shahada ya Heshima ya Uzamivu katika Uchumi. Nawashukuru kwa heshima hii kutoka kwa chuo kikuu hiki maarufu, kilichopo kwenye nchi ambayo elimu yake inachukuliwa kuwa ni ya daraja la juu duniani,” amesema Dk. Samia.

Rais Samia pia anatarajiwa kuelekea jijini Istanbul, mji mkuu wa kibiashara wa nchi ya Uturuki kushiriki Kongamano la kibiashara la Tanzania na nchi hiyo linalotarajiwa kuhudhuriwa na Makamu wa Rais wa Uturuki.