Urusi yashambulia miundombinu ya nishati ya Ukraine

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:05 PM Apr 28 2024
Sehemu ya athari ya shambulizi la kombora la Urusi.
Picha: Stringer/Anadolu/picture alliance
Sehemu ya athari ya shambulizi la kombora la Urusi.

URUSI imeishambulia Ukraine kwa makombora usiku kucha na kuharibu vituo vinne vya kuzalisha umeme, katika mkururo wa mashambulizi ya hivi karibuni unaolenga miundombinu ya nishati.

Waziri wa nishati wa Ukraine, German Galushchenko amevitaja vituo vilivyoathirika kuwa ni katika mikoa mitatu ya Lviv, Ivano na Frankivsk magharibi, kilomita kadhaa kutoka mstari wa mapambano. 

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ametoa wito kwa washirika wake wa nchi za Magharibi kutuma silaha zaidi za mifumo ya ulinzi wa anga, ili kuilinda nchi yake wakati ambapo jeshi la anga la nchi likidai kudungua makombora 21 kati ya 34 yaliyofyatuliwa kuelekea nchini humo.

Kwa upande wake Ukraine nayo ilirusha zaidi ya droni 60 kuelekea upande wa kusini mwa Urusi, huku Moscow ikisema kuwa lilikuwa moja ya shambulizi kubwa la droni la usiku kucha.

DW