ACT Wazalendo: Hatuko tayari kuhujumiwa uchaguzi ujao Zanzibar

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 09:34 AM Apr 28 2024
Waziri Mkuu Kivuli, Isihaka Mchinjita.
PICHA: ACT WAZALENDO
Waziri Mkuu Kivuli, Isihaka Mchinjita.

CHAMA cha ACT Wazalendo, kimesema wakati taifa linapoelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao, hakiko tayari kushuhudia hujuma za uchaguzi, kisha kusubiri wale waliowahujumu waje mbele yao wameinamisha shingo.

Aidha, kimetoa wito kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, asijiingize kwenye orodha ya marais, ambao katika zama zao walishiriki kumwaga damu ya Wazanzibar.

Akizungumza katika Mji wa Moshi, mkoani Kilimanjaro, wakati wa mkutano mkuu wa kidemokrasia wa ACT Wazalendo (MMK) na miaka 10 ya mapambano na matumaini, Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bara, ambaye pia ni Waziri Mkuu Kivuli, Isihaka Mchinjita, amesema ACT Wazalendo inajiandaa kwenda kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, na wanakwenda kuiongoza Serikali ya Zanzibar.

“Ni vyema sana Rais (Dk. Hussein) Mwinyi asijiingize kwenye orodha ya marais ambao katika zama zao walishiriki kumwaga damu ya Wazanzibar. Huu ndio wito wetu ACT Wazalendo tunautoa kwa Rais Mwinyi.

“Namweleza wazi kwamba, hatuko tayari kushuhudia hujuma za uchaguzi kisha kusubiri wale waliotuhujumu waje mbele yetu wameinamisha shingo kana kwamba hakuna walichofanya,”  amesema.

Kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Uchaguzi na Tume Huru ya Uchaguzi, Mchinjita  amesema hawana tatizo la maoni yaliyotolewa na Kikosi Kazi cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwa yapo na yamewekwa hadharani na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Samia Suluhu Hassan), na leo unaweza kwenda kuyaona.

Hata hivyo,  amesema shida yao ni maoni ya Kikosi Kazi cha Zanzibar, akidai yameshikiliwa na hayajafanyiwa kazi.

“Nataka niwaambie wana mabadiliko wote, na wapigania demokrasia Zanzibar. ACT Wazalendo, itashirikiana nao kuhakikisha kwamba mabadiliko yanafanyika,”  amesema.

Katika ufunguzi wa kongamano hilo, Kiongozi mpya wa Chama Cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, akieleza hali ya nchi kiuchumi kwa miaka 10, akiyataja mambo matano yanayotakiwa kudhibitiwa ili kuliepusha taifa kufarakanika na kuendeleza utegemezi, hata
baada ya miaka mingi ya uhuru wa kisiasa.

“Mambo ambayo tulieleza yanayoitafuna nchi yetu na kufuja rasilimali za umma ni kama vile ufisadi mkubwa unaotegeneza mabilionea na kuwaacha maskini mamilioni, utoroshwaji wa fedha unaofanywa na kampuni za kimataifa (illicit financial outflow) tafiti zinaonesha
Tanzania inapoteza fedha wastani wa shilingi trilioni 2.1 kila mwaka. 

“Sehemu kubwa inafanywa na Kampuni za Kigeni na na sehemunyingine nibakshishi wanayopewa viongozi namaafisa wa serikali wanaofanikisha utoroshaji huu. Vilevile, uingiaji wa mikataba ya madini, gesi, mafuta na uwekezaji mwingine bila kuzingatia uhitaji
wakuboresha mazingira ya nchi kufaidikana utajiri wa rasilimali zetu.

“Wizi mkubwa na ubadhirifu wa fedha za umma unaoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG); Kutokuwa na sawa kimaendeleo kati ya mijini na vijijini (Mfumo wa maendeleo unao wanyonya wananchi walio wengi vijijini),”  amesema.

Ameongeza kuwa: “Kwa ufupi, miaka 10 ya uwapo wetu kama chama cha siasa tunaendelea kuona sera zisizo za kizalendo zikitekelezwa na Serikali ya CCM. Sera zisizojali maslahi ya walio wengi badala yake viongozi wa kisiasa na umma kwa ujumla wanatumia mwanya kujiimarisha katika maslahi binafsi dhidi ya maslahi ya umma na hivyo kuzima ndoto za ujenzi wa Taifa la watu wote.

“Pamoja na kwamba nchi yetu imejaliwa rasilimali nyingi, raia wake kwa umoja wao hawafaidiki na rasilimali hizi lakini zinaendelea kuwaneemesha watu wachache walio Serikalini, Mashirika ya Umma na Kampuni za kimataifa. Bado, uchumi wa taifa huru unaendelea kuwatajirisha watu wa nje na wachache wa ndani ya nchi huku mamilioni ya watanzania wakifukarishwa. Tunaweza kuona viashiria kadhaa vya hali ya nchi yetu kiuchumi sio nzuri na hatuelekei pazuri.”

Amevitaja viashiria hivyo kuwa ni, kasi kubwa ya ukuaji wa deni la serikali, suala la huduma za afya na kupaa kwa gharama za matibabu, ukosefu wa ajira na kipato cha uhakika, kikotoo cha mafao kwa wastaafu na hali ngumu ya maisha na hali ya umaskini.

Amesema katika picha ya jumla, hali hii ya kiuchumi inawaonyesha kuwa bado mapambano yao ya kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika na zinalitufaifa taifa (kwa maslahi ya wote na sio wachache wale wale), yanapaswa kuendelea na kuongezewa nguvu mara dafu sasa, kuliko wakati mwingine katika historia ya chama chao.

Kwa mujibu wa Semu, ACT-Wazalendo kinapaswa kuongoza umma kwa ajili ya kufufua utaifa wa Tanzania, ili kila Mtanzania aone kuwa ana wajibuwa kujenga nchi yake ili kutimiza ndoto ya kuwa na taifa lenye kujitegemea kiuchumi na kiutamaduni; na ambalo lina linda na
kudumisha usawa, ustawiwa jamii, uwajibikaji, demokrasia na uongozi bora.