Ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kumuua shangazi

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 05:03 PM Apr 18 2024
Ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kumuua shangazi yake.
PICHA: MAKTABA
Ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kumuua shangazi yake.

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Shinyanga imemuhukumu kunyongwa hadi kufa, Alex Masanja mkazi wa Mwigumbi wilayani Kishapu mkoani hapa kwa kosa la kumuua shangazi.

Ilielezwa mahakamani hapo kwamba Februari 16 mwaka jana mtuhumiwa alimpiga shangazi yake, Melisiana Malisa mkazi wa Kijiji cha Masagara wilayani Kishapu na kitu kizito kichwani baada ya kumzuia kutumia baiskeli yake.

Ilielezwa kuwa baada ya kutekeleza mauaji hayo mtuhumiwa aliiuza na kukimbilia kujificha wilayani Sikongwa mkoani Tabora kwa mganga wa kienyeji.

Akisoma hukumu hiyo yenye Shauri Namba 54 la Mwaka 2023, Jaji Seif Kulita alisema February 16 mwaka jana majira ya usiku Melisiana (marehemu) akiwa amelala alivamiwa na kupigwa na kitu kizito kichwani na mwili wake ulikutwa na majeraha kichwani pamoja na kuvuja damu.

Aidha, upande wa utetezi wa shauli hilo ukiongozwa na wakili Emmanuel Ruugamila akizungumza baada ya hukumu kutolewa alisema wameipokea hukumu kama ilivyosomwa.

Alisema hukumu hiyo haimzuii mshitakiwa kutokukata rufaa, endapo itaonekana kuna haja ya kufanya hivyo japokuwa hukumu ya kunyongwa hadi kufa ni adhabu kubwa ambayo uwezi kuomba ufanye utetezi wa aina nyingine

"Tumepokea jinsi ambavyo Mahakama ilivyochambua na kutoa maamuzi, hakuna kesi ndogo kesi zote ni kubwa, lakini inategemea na ushahidi uliotolewa, mfano kesi hii ushahidi uliotolewa ulikuwa wa kimazingira lakini kwa sababu uliungwa mkono na mashahidi walioletwa na Jamhuri ndio maana Mahakama imeweza kufikia maamuzi haya " alisema Ruugamila.

Aidha, wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka mkoani hapa, Mboneke Ndimubeya alisema hukumu hiyo ni mafanikio makubwa kwao kwa sababu imeonyesha dhahili upande wa mashitaka wameweza kuthibitisha kosa la mauaji pasipo kuacha shaka yoyote.

Alisema mshitakiwa amepewa hukumu hiyo kutokana na ushahidi wa kimazingira ambao umejitosheleza moja kwa moja na unamgusa yeye ukiambatanisha na ungamo alilolifanya kwa hakimu.