Aliyepinga kifungo miaka 30 kwa kubaka, afungwa maisha

By Kulwa Mzee , Nipashe
Published at 03:57 PM May 02 2024
Afungwa jela maisha kwa ubakaji.
PICHA: MAKTABA
Afungwa jela maisha kwa ubakaji.

MAHAKAMA Kuu Masijala ya Moshi imemuhukumu kifungo cha maisha jela, Elineema Mwandry, aliyekata rufani akipinga adhabu ya miaka 30 jela aliyopewa na Mahakama ya Wilaya ya Siha kwa kumbaka binti yake akiwa na miaka saba.

Mwandry ameongezewa kifungo na mahakama hiyo mbele ya Jaji Lilian Mongela baada ya kutupilia mbali rufani ya kupinga hukumu ya mahakama ya chini.

Ilidaiwa Mei 14, 2022 kijiji cha Lomakaa wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro, mrufani alidaiwa kumbaka binti yake mwenye umri wa miaka saba ambaye anasoma darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Lomakaa.

Mrufani aliposomewa mashtaka alikana kutenda tukio hilo, upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi watano na upande wa utetezi mrufani alikuwa na shahidi mmoja.

Ilidaiwa mara nyingi mrufani alikuwa anatumia chumba cha kulala wageni kumwingilia binti yake.

Mei 16, 2022 binti alitoa taarifa ya tukio hilo kwa rafiki yake ambaye ni shahidi wa pili na yeye alimshauri akatoe taarifa kwa dada mkuu wa shule hiyo.

Shahidi huyo pia alimshauri akatoe taarifa kwa mwalimu wa darasa ambaye ni shahidi wa tatu alifanya hivyo na shahidi huyo wa tatu pia alitoa taarifa kwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ambaye ni shahidi wa nne.

Baada ya taarifa hizo kufika kwa uongozi wa shule walitoa taarifa Polisi na Mei 23, 2022 mrufani alikamatwa na kushtakiwa kwa kubaka.

Shahidi wa tano ambaye ni daktari alimfanyia uchunguzi binti na kubainisha katika ripoti yake kwamba aliingiliwa na kitu kutokana na sehemu ya siri kuongezeka ukubwa.

Katika utetezi wake mrufani alidai hakuwa akiishi na mama wa binti huyo ambaye alimwambia atakuja kumfanyia kitu kibaya ambacho hatakisahau.

Alidai kesi hiyo imetengenezwa hakuwahi kufanya tukio hilo.

Akipinga adhabu ya miaka 30 jela aliyopewa na Mahakama ya Wilaya ya Siha baada ya kumtia hatiani alitoa sababu nne.

Alidai Mahakama ilikosea kumuhukumu na kumtia hatiani wakati hakukuwa na uthibitisho wa umri halisi wa mtoto, ilikosea pia kuegemea katika ushahidi wa shahidi wa kwanza na wapili.

Alidai Mahakama ilikosea kumtia hatiani kwa mashtaka ambayo hayakuthibitishwa bila kuacha shaka na upande wa Jamhuri na kwamba Mahakama hiyo haikuzingatia utetezi wake wakati inatoa hukumu.

Mahakama baada ya kusikiliza hoja hizo na majibu ya Wakili wa Serikali Henry Daudi, ilitoa uamuzi.

"Kuhusiana na ushahidi wa shahidi wa pili unaodaiwa kukinzana na ushahidi wa shahidi wa kwanza, ningependa kusema kwamba sio mikanganyiko yote inaweza kuathiri ushahidi katika kesi.

"Katika suala lililopo mbele yetu, shahidi wa pili taarifa yake ilikuwa kuhusiana na kile shahidi wa kwanza alikuwa amemwambia. 

"Kwa wazi huo ulikuwa uvumi, hakuwahi kuwapo kwenye tukio lolote ambapo shahidi wa kwanza iliingiliwa na mrufani. 

"Kwa kweli, sioni madai ya kupingana na chochote kilichosemwa na mwathiriwa kuhusu ubakaji, matukio yaliyofanywa kwake na mrufani.

"Katika ushahidi uliotangulia, nina maoni kwamba mahakama ya chini ilimtia hatiani mrufani, kama ilivyoelezwa na Wakili Daudi, hukumu haikuwa sahihi kwa mujibu wa Kifungu cha 131(3) cha Kanuni ya Adhabu.

"Adhabu kwa ubakaji wa msichana chini ya miaka kumi ni kifungo cha maisha jela lakini Mahakama ya chini ilimhukumu mrufani kifungo cha miaka 30 jela.

"Mahakama inaongeza adhabu, mrufani atatumikia kifungo cha maisha jela kwa mujibu wa Kifungu cha 131(3) cha Kanuni ya Adhabu," alisema Jaji Mongela.