Biteko ataka orodha taasisi zinazodaiwa na vyombo vya habari

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 10:00 AM Apr 30 2024
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko.
PICHA: MAKTABA
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko.

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko, amemwagiza Waziri wa Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Nape Nnauye, kumpa orodha ya taasisi za serikali zinazodaiwa na vyombo vya habari ili madeni hayo yaanze kulipwa.

Dk. Biteko ametoa agizo hilo jijini hapa alipokuwa akifungua mkutano wa 13 wa kitaaluma wa wahariri wa vyombo vya habari nchini, ulioandaliwa na Jukwaa la Wahariri (TEF).

Amesema madeni ambayo serikali inadaiwa na vyombo vya habari yanapaswa kufanyiwa kazi ili yalipwe kuanzia sasa.

"Waziri haya madeni naomba uniandikie kwa maandishi ili nijue nani anadaiwa, lakini kwa kiasi gani ili vyombo vya habari vianze kulipwa. Mtu anaweza asiwe na uwezo wa kulipa deni lote, lakini aseme atalipaje na kwa kiasi gani." 

Aidha, amevitaka vyombo vya habari nchini kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na busara kwenye uandishi wa habari.

"Tunapotoa habari zetu tuangalie pia maslahi mapana ya taifa kweli inaweza kuwa ni habari lakini lazima busara itumike ili kulinda maslahi mapana ya taifa letu," amesisitiza.

Amelipongeza Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kwa ubunifu na kuja na lengo la kutumia vyombo vya habari kuhamasisha matumizi ya gesi ili kulinda misitu nchini.

Amesema serikali imeweka jitihada kubwa katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kuondokana na nishati chafu za kuni na mkaa.

Awali, Waziri wa Habari, Tekonolojia ya Habari na Mawasiliano, amesema madeni ya serikali yanachangia kuua baadhi ya vyombo vya habari nchini.

"New Habari nasikia walifunga gazeti na walikuwa na mtambo kabisa wa kuchapisha magazeti, lakini kutokana na madeni walifunga gazeti. Hivyo nikuombe kaka yangu Naibu Waziri Mkuu madeni haya serikali yalipwe hata uwekwe utaratibu fulani wa kuyalipa," amesisitiza Waziri Nape.

Vile vile, amesema ripoti ya hali ya uchumi wa vyombo vya habari ipo tayari na wataitoa muda wowote kuanzia sasa.

Naye Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, amesema hivi sasa hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchi inaridhisha kwa kiasi kikubwa.