CEOrt yazindua mpango wa kuongeza wanawake katika uongozi

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 07:12 PM Apr 18 2024
Naibu Waziri wa Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wanawake na makundi Maalum, Mwanaidi Ali Hamis.

Kampuni ya CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) imezindua mpango ‘Think Equal Lead Smart’ (TELS), mradi wa awali wa miaka mitatu ulioundwa ili kukuza ushiriki kamili na wenye tija wa wanawake kupitia uundaji wa fursa sawa za uongozi katika majukwaa yote ya maamuzi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo jijini Dar es Salaam leo Naibu Waziri wa Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wanawake na makundi Maalum, Mwanaidi Ali Hamis, amesema Wanawake wana mchango mkubwa katika maendeleo ya familia na Taifa kwa ujumla, hasa ikizingatiwa kuwa kundi kubwa la watu hapa nchini ni Wanawake.

Amesema pamoja na hayo bado wanawake wanakabiliwa na changamoto zinazowaathiri na kuwakwamisha katika maendeleo yao ikiwemo mila na destruri zenye madhara, kutopatiwa fursa ya kupata elimu pamoja na kutoshirikishwa katika shughuli za ujasiriamali na uzalishaji mali.

''Kwa namna ya pekee naupongeza Uongozi wa Taasisi hii kwa kuendelea kutambua umuhimu wa wanawake na vijana kushiriki katika nafasi za uongozi na maamuzi, nyie ni taasisi ya mfano wa kuigwa kwa maendeleo ya Wanawake, na sisi Serikali tunaunga mkono juhudi hizi za kumkwamua mwanamke'', amesema 

Amesema  kinachofanywa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na washirika wao ni kuunga mkono dhamira ya Rais wa Samia Suluhu Hassan ya kutoa nafasi zaidi ya uongozi kwa wanawake jambo alilolifanya baada ya kuchukua uongozi wa nchi.

''Hivi sasa, takwimu zinaoenesha kuna ongezeko la Mawaziri Wanawake kutoka asilimia 15 kwa mwaka 2005 hadi asilimia 37 kwa mwaka 2023, aidha, Wabunge wanawake wameongezeka kutoka asilimia 22 hadi kufikia asilimia 37 kwa mwaka 2023.

Pamoja na hao, pia Wanawake Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wapo asilimia 38, Madiwani asilimia 29.9, Mabalozi asilimia 25, Makatibu Wakuu asilimia 22, Naibu Katibu Wakuu asilimia 28, Wakuu wa Mikoa asilimia 31, Makatibu Tawala asilimia 26, Wakuu wa Wilaya asilimia 33 na Wakurugenzi asilimia 28, kwa ujumla haya ni mafanikio makubwa sana kwa wanawake katika kushika nafasi za uongozi na za maamuzi hapa nchini,'' amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt, Santina Benson amesema mpango huo unalenga kuongeza idadi ya viongozi wanawake katika majukumu yote ya maamuzi, na kuongeza kuwa takwimu za soko la hisa zinaonyesha kuwa kati ya kampuni 28 kuna mtendaji mmoja mwanamke, ambayo ina maana kwamba lengo lililowekwa kuwa na viongozi wengi wanawake katika sekta binafsi haijafikiwa.

"Tunatambua jukumu muhimu la wanawake katika kuendeleza maendeleo endelevu na ukuaji shirikishi. Kupitia mpango wa TELS, tunalenga kuleta pamoja washikadau wenye ujuzi sahihi wa kiufundi ili kuongeza uelewa wa changamoto za ukosefu wa usawa wa kijinsia ndani ya maeneo muhimu ya kuzingatia na kuandaa masuluhisho ya kuimarisha ushirikishwaji wa kijinsia,” amesema.

Santina, amesema kwamba mafanikio makubwa yamepatikana katika kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake nchini, bado kuna kazi kubwa ya kuwapatia wanawake fursa sawa za uongozi.

“Tunakiri kwamba hadi sasa, kuna idadi ya programu zinazolenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi. Hata hivyo, lengo la kipekee la mpango huu ni kuendesha mabadiliko ya kimfumo. Matokeo ya mwisho yanayotarajiwa ni mabadiliko katika miundo ya shirika, sera na matendo ya taasisi, na kuona moja kwa moja mabadiliko katika ngazi zote za jamii,” amesema.

Mwenyekiti wa Vodacom Foundation, Harriet Lwakatare amesema Vodacom kama wafadhili wakuu wa malengo ya mradi huo kusaidia mpango wa CEOrt kupitia utaalam wa kifedha, na kuongeza kuwa hiyo pia ni fursa ya kuwafikia watu wengi zaidi.