DC Mhita atoa ya moyoni kuhusu mafuriko Igwamanoni

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 05:34 PM Apr 18 2024
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita akikagua moja ya vyumba vya madarasa vitano vilivyotitia na kuwa na nyufa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
PICHA: SHABAN NJIA
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita akikagua moja ya vyumba vya madarasa vitano vilivyotitia na kuwa na nyufa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

MKUU wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita amefika na kukagua maeneo yaliyoathirika na mafuriko, yaliyotokana na mvua za masika katika Kata ya Igwamanoni, Halmashauri ya Ushetu, mkoani Shinyanga.

Mafuriko hayo yamesababisha Shule ya Msingi Igwamanoni kufungwa kwa muda usijulikana, hasa baada ya baadhi ya madarasa katika shule hiyo kutitia, huku kuta zake zikiwa na nyufa.

Aidha, kaya 533 zimeathirika na mvua hiyo kwa kupata nyufa mbalimbali na kulazimika kuhama na kuelekea sehemu zenye usalama hususani katika shule ambazo hazijathirika, ofisi za Serikali za vijiji na zile za kata huku kukiwa hakuna vifo wala majeruhi yaliyojitokeza.

Akizungumza mara baada ya kujionea athari hizo Mhita amesema, aina ya udongo ya ardhi ya halmashauri hiyo ni udongo unao hifadhi sana maji na kwamba mvua zinazonyesha ardhi imejaa maji na kuyatapika hivyo na kusababisha barabara nyingi kukatika na nyumba kupata nyufa kwa kutitia.

Pia amesema, asilimia kubwa ya nyumba zilizoathiriwa ni zile zilizojengwa kwa kutokuzingatia vigezo vya ujenzi kwani nyingi hazina msingi imara, barabara kutokuwa na mitaro na wataendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kupunguza athari na madhara ya mvua.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Hadija Kabojela amesema, tayari wameshaanza kutoa elimu ya kujikinga na athari za mvua kwa wananchi, sambamba na kuchukua hatua mbalimbali za tahadhari kwa wananchi ambao wameathiriwa na mafuriko haya na mpaka sasa hakuna majeruhi wala vifo virivyoripotiwa.

“April 10 ya siku ya Eid Alfitr kulinyesha mvua kubwa sana kwa zaidi ya masaa manne na kusababisha barabara nyingi kukatika, nyumba kupata nyufa na madarasa ya shule ya msingi Igwamanoni matavo yanayotumiwa na wanafunzi kutitia na kupata nyufa na hii imesababisha kuwahamisha shule jirani ya Iramba ili waendelee na masomo yao” Amesema Kabojela.