Diwani, mkandarasi watunishiana misuli mbele ya Mbunge

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:18 AM May 09 2024
Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo.
Picha: Maktaba
Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo.

DIWANI wa Kata ya Muriet ya Halmashauri ya Jiji la Arusha, Francis Mbise na mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi ya Hari Singh & Sons Limited, aliyepewa zabuni ya ujenzi wa barabara za kata hiyo kwa kiwango cha changarawe, wametunishiana misuli’ hadharani, kisa Sh.600,000 za kuwekewa moramu kutotumika kama walivyokubaliana.

Tukio hilo limetokea mbele ya Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo, aliyekuwa amekwenda kwenye kata hiyo kukabidhi gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya Muriet.

Inaelezwa kwamba Diwani Mbise, amempa mkandarasi huyo fedha hizo kwa ajili ya kuweka moramu barabarani ili kuharakisha mradi huo wa ujenzi, kitu ambacho hakutekeleza.

"Ninavyoongea hapa, nikimaliza nataka pesa yangu irudi niliyotoa kwa ajili ya kuweka moramu kwenye hii barabara. Baada ya kuona mambo ya ujenzi hayaendi, matokeo yake pesa sioni na kazi haifanyiki.

“Kama mpaka mimi mmenirusha pesa yangu, je, hii barabara itakamilika kwa wakati kweli? Alihoji Mbise, huku akisisitiza kurudishiwa fedha hizo.

Kwa mujibu wa diwani huyo, tangu alipomkabidhi mkandarasi fedha hizo ambazo wananchi wake walichangishana, hakuna kilichofanyika zaidi ya kuwekewa mitambo na kutelekezewa katika barabara.

Alipoulizwa kuhusiana na madai hayo, mkandarasi aliyekuwapo katika eneo hilo la mradi, Stephen Mhauka, amesema aliyechukua fedha hizo kwa Diwani huyo ni mfanyakazi wake, aliyemtaja kwa jina moja la Innocent, huku akiahidi kumtafuta ili arejeshe.

Amesema mkataba wao katika mradi huo, unafikia ukomo Juni 15, mwaka huu, lakini kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, ameomba kuongezwa muda hadi Julai mwaka huu. 

Wakati wa majibishano hayo, Gambo alikuwa akiendelea kusikiliza kero za wananchi baada ya kukabidhi gari hilo la wagonjwa kwa kituo hicho cha afya.