Gekul ang’ang’aniwa akatiwa rufani

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 10:00 AM May 07 2024
MBUNGE wa Babati Mjini (CCM) na Naibu Waziri wa zamani wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul.
PICHA: MAKTABA
MBUNGE wa Babati Mjini (CCM) na Naibu Waziri wa zamani wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul.

MBUNGE wa Babati Mjini (CCM) na Naibu Waziri wa zamani wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul, ameendelea kung’anga’niwa baada ya mlalamikaji katika kesi ya udhalilishaji kuweka kusudio la kukata rufani dhidi ya ushindi aliopewa na mahakama.

Mlalamikaji katika kesi hiyo ni aliyekuwa mfanyakazi wake, Hashim Ally, ambaye kupitia wakili wake, Peter Madeleka, amewasilisha rufani namba 5502749 ya mwaka 2024 iliyosajiliwa katika Masijala ya Manyara kwa kutumia mtandao wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mei 5, mwaka huu.

Hashim, anapinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara, uliotolewa na Jaji Devotha Kamuzora, Aprili 15 mwaka huu, kutupilia mbali kesi dhidi ya mbunge huyo.

Wakili Madeleka kutoka Kampuni ya Stalwart Law Chambers, anayemtetea Hashim Ally, akizungumza na gazeti hili amesema tayari mteja wake amefungua kesi hiyo.

Aprili 15, mwaka huu katika Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara, Mbunge Gekul, ameshinda kesi ya rufani ya udhalilishaji iliyofunguliwa na mfanyakazi wake, Hashim, baada ya Jaji Kamuzora, kueleza ilani iliyotumika kumfungulia kesi ya msingi, haikukidhi vigezo.

Katika kesi ya msingi, Gekul alikuwa akikabiliwa na shtaka moja la shambulio na kusababisha madhara ya mwili, chini ya kifungu cha 241 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa Marejeo mwaka 2022.

Amedai kuwa yeye na watu wengine ambao hawako katika malalamiko hayo, Novemba 1, 2023, Mjini Babati, mkoani Manyara, walimuita Hashim na kumweka kizuizini.

Amedai huku wakimtishia kwa silaha ya moto, walimvua nguo na kumshambulia kwa kumlazimisha kukalia chupa ya soda ili iingie katika njia yake ya haja kubwa, jambo lililomsababishia madhara.